05 Jun 2020 Reportaje

Tutunze mazingira kwa hali na mali

Ni zaidi ya miaka mitatu tangu Kenya ilipopiga marufuku matumizi ya baadhi ya mifuko ya plastiki kwenye jitihada za kutunza mazingira. Ni jambo ambalo limeifanya Kenya kujizolea sifa kocho kocho kote ulimwenguni.

Sote tunajivunia hatua hii. Na ingawa tumeshuhudia mabadiliko mengi na mazuri kimazingira, kuna hatua zaidi ambazo zinapaswa kuchukuliwa ili kuboresha hatua hizi, kwa kuwa tumeendelea kuona uchafuzi kutokana na aina zingine za plaskiti kama chupa za maji, mirija, mifuko na nyinginezo; plastiki ambazo zinatumika mara moja tu.  

Ni jambo la busara kwa Kenya kupiga marufuku aina fulani za plastiki katika maeneo yaliyohifadhiwa. Hata hivyo, tusisahau kuwa wakati mwingi uchafu wa plastiki hubebwa na upepo na pia kusafirishwa na maji ya mvua na mito hadi maeneo hayo. Ikiwa tutamaliza uchafu huu wa plastiki, itabidi tuangazie suala zima.

Kulingana na ripoti ya hivi majuzi, kuna uwezekano mkubwa kwa uchafu wa plastiki kuzika samaki baharini. Hili linatia hofu. Vilevile, ni shinikizo kwa serikali kukaza kamba kutunza mazingira.

Kampuni ambazo huunda na kutumia plastiki zinapaswa kuwa katika mstari wa mbele kuona kuwa plastiki zao hazichafui mazingira ila zinaokotwa na kurejereshwa. Sio tu kuwekelea lawama wateja wao ambao wakati mwingi hawana uelewa mwema wa kuhifadhi plastiki ambazo wamemaliza kuzitumia. Hivyo basi, ni lazima kampuni hizi kuwajibika katika kutunza mazingira, la sivyo sheria mwafaka zipitishwe ili kampuni hizi ziajibike. 

Tunaposherehekea siku ya Mazingira Duniani mwaka huu, ambapo kaulimbiu ni: ‘Bayoanuai.’  tunastahili kutambua kwamba, kamwe hatuwezi kuishi duniani peke yetu. Yahitaji ushirikiano baina yetu na viumbe wote. Kila kiumbe kina umuhimu wake hapa duniani.

Ni jambo la kutia hofu tunapowaona wawindaji haramu wakiwaua wanyama wa porini ili wajinufaishe wenyewe. Kuna uwezekano virusi vya korona ambavyo vimekuwa tisho kuu duniani vilitoka kwenye soko la kuuza viungo vya wanyama pori. Ikiwa basi tutaishi bila maradhi ibuka, sharti tutunze mazingira kwa hali na mali. La sivyo, tutaendelea kuteseka kutokana na mikurupuko ya magonjwa ambayo hayaeleweki.

Uharibifu wa mazingira ambao unahatarisha viumbe hai unastahili kuchukuliwa kama makosa makubwa dhidi ya wanadamu. Wazo ambalo mataifa mengi yamekuwa yakishinikiza, eti hakuna maendeleo pasi uchafuzi ni potovu.

Maendeleo ni muhimu kwa kila nchi lakini, zahitaji kutumia njia safi ambazo hazidhuru mazingira kiwango cha kuhatarisha binadamu na viumbe wengine. Kwa mfano uchomaji taka za plastiki umeonekana kuchangia kmaradhi ya vifua, maradhi ya moyo na hata saratani.

Kuna baadhi ya watu binafsi, makundi na mashirika ambayo yamemakinika katika kuzoa taka za plastiki katika mazingira na kuzigeuza kuunda vitu vyenye thamani.Mwaka jana, shirika la Flip Flopi, likiongozwa na Bw Ali Skanda, ambaye ni fundi wa mashua za kale, lilitengeneza mashua kwa kutumia taka za plastiki ambazo zilichakatwa. Bw Skanda pia ni mwanzilishi wa Wakfu wa TakaTaka.

Baadaye, chombo hicho kiling’oa nanga kutoka Lamu hadi Zanzibar, ambako ni umbali wa kilomita 500, kwenye juhudi za kuelimisha watu wa Pwani kuhusu athari za plastiki baharini. Mwaka huu, shirika la Flip Flopi, likishirikiana na wapenzi wa mazingira, linaendelea kuomba Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kupiga marufuku plastiki za matumizi ya mara moja tu.

Hili ni kutokana na uchafuzi unaondelea katika Ziwa Victoria. Sote tunapaswa kuwajibika kutunza mazingira kwa minajili ya vizazi vya leo na vya kesho.

 

Mwandishi

James Wakibia, Mwanaharakati wa Mazingira.