02 Mar 2020 Tukio Misitu

Jinsi ambavyo Mshindi wa Tuzo la Mazingira nchini Kenya anavyopanda miti katika mji anaotoka.

Tunapoelekea Siku ya Wanawake Duniani, Shirika la wanawake la Umoja wa Mataifa linajivunia watu wote waliochukua hatua za kufanya dunia kuwa na usawa wa kijinsia unaohitajika bila kubagua jinsia, umri, kabila, dini au taifa. Kutana na mtu wa sampuli hii kutoka Kenya.

Joan Tonui alikuwa na umri wa miaka 22 tu alipotuzwa Tuzo la Mazingira huko Bomet. Aliambia jopo la waamuzi kuwa alitaka kufanya kazi na wanawake na watoto ili kuwahamasisha kuhusu umuhimu wa kuishi katika mazingira safi na kuwafundisha jinsi ya kushughulikia taka katika maeneo ya mjini. Akiwa amesomea masuala ya afya ya umma, hasa maji na usafi, alijifunza jinsi ambavyo baadhi ya nchi hutenga takataka zao kwa makundi, kwa mfano glasi, plastiki na makaratasi, na alitaka dhana hii ifundishwe katika shule zinazopatikana katika eneo analoishi.

Alianza kutembelea shule na kuzungumzia kuhusu mradi wake. Hakuzungumzia tu jinsi ya kushughulikia taka ila aliwahimiza kukuza miche ili kupata matunda na mbegu ya miti ya kiasili itakayowezesha wanajamii kupanda shuleni baadaye. Mradi huu ulizalisha 'Programu ya Mabingwa wa Kijani' ambapo huwa anaandaa mashindano, na mwanafunzi aaliyebobea zaidi kwa masuala ya mazingira kupitia ushauri, insha, michoro na michezo ya kuigiza inayofanywa shuleni hutuzwa tuzo la 'Green Champion'.

Lengo ni kuwafanya hawa mabingwa kushawishi wengine kujiunga na 'Green Champions Club'.  Wanachama wa klabu hiyo hutunza vitalu na kuandaa 'green days' shuleni huku wakifanya shughuli kama vile kukusanya taka au kupanda miti. Kila mwanafunzi hujichukulia mti, kuupa jina na kuutunza hadi utakapokua. Wanapomaliza kusoma hurithisha mwanafunzi mwingine.

"Kufikia sasa, nimeweza kuanzisha mradi huu katika shule za msingi kadhaa katika Kaunti ya Bomet, ila nina nia ya kuusambaza kwa kaunti zingine," asema Tonui.

img
Sumaya, mwenye umri wa miaka 10 pia huwaimiza wazazi wake kupanda miti.

"Hata watu wakikata miti, hakuna anayekuzuia kupanda tena. Mimi hufanya hivyo mara kwa mara," asema Sumaya, mwenye umri wa miaka 10. Pia, ameshawishi wazazi wake kupanda miti zaidi. "Miti huzuia mmomonyoko wa udongo na pia ni makaazi ya wanyama. Isitoshe, hurembesha mazingira.

Walinda mito

Mbali na kufanya kazi na wanafunzi shuleni, Tonui huhamasisha vijana na wanawake wanaoishi karibu na mito. Yeye huwarejelea kama Walinda Mito wake. Ni watu wanaonafanya kazi bila malipo na hupanda miti mingine na kuondoa mikalutusi inayohatarisha Mto Mara na kuchangia hali ya ukame.

"Niliomba ruhusa kutoka kwa machifu na wazee wa mtaa ili kuuliza wanakijiji kujitolea kufanya kazi nami ili kung'oa mikalitusi na kupanda mianzi na miti ya kiasili kama vile miparachichi. Kwa upande mwingine, huwapa mafunzo kuhusu njia mbadala ya kipato kama vaie kushona vikapu kwa kutumia matawi ya mienezi. Watu hao wanaofanya kazi bila malipo hudokeza kuhusu yale ambayo wangependa kujifunza. Kwa hivyo, ufugaji wa nyuki ulioongezwa katika programu yetu," anaelezea.

Kwa kipindi cha miezi sita tu, ameweza kujumuisha vijiji tano kwa sababu wanaelewa manufaa ya kudumu ya kutunza mito.

"Ni sharti tushirikiane na mazingira, tusiyabughudhi, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi," anasemaTim Christophersen, Msimamizi wa Idara ya 'Mbinu Asili za Kutunza Mazingira' wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa. "Masuhuhisho ya kiasili yanaweza kuleta ustahimilifu, kupunguza hewa ya ukaa, kuboresha afya na kuwezesha wakulima kupata riziki. Kwa Shirika la Umoja wa Mataifa, misitu na mifumo mingine muhimu ya ekolojia ni muhimu wakati wa kuweka mikakati ya kufikia maendeleo endelevu, na sisi hutumia programu zetu kama vile UN-REDD na ile ya Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia kufanya kazi kwa ushirikiano na wadau wote walio tayari kujiunga nasi.”

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na Ingrid Dierckxsens.

Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia  kuanzia mwaka wa 2021 hadi mwaka wa 2030, ukiendeshwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano na wabia kama vile 'Africa Restoration 100 initiative', 'Global Landscapes Forum' na Muungano wa Kimataifa wa Utunzaji wa Mazingira, hushughulikia mifumo ya ekolojia katika maeneo ya nchi kavu na maneo ya bahari. Wito unatolewa kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua, itapokea msaada kutoka kwa wanasasia, watafiti wa kisayansi na msaada wa kifedha ili kuboresha kwa kasi. Tusaidie Kuimarisha Muongo Huu.