Katika mwaka wake wa kwanza, Kituo cha Kimataifa cha Kufuatilia Uzalishaji wa Methani Duniani (IMEO) cha UNEP kilitekeleza wajibu muhimu kusaidia kupunguza uzalishaji wa methani, kichocheo cha pili kwa ukubwa cha ongezeko la joto duniani. Kituo hiki kilianzishwa ili kusaidia kufikia malengo kama vile Ahadi za Methani Duniani za kupunguza asilimia 30 ya uzalishaji wa methani katika sekta ya mafuta na gesi, sekta ya kilimo na taka kufikia mwaka wa 2030. Kufikia Novemba mwaka wa 2022, nchi 150 zilikuwa zimeidhinisha ahadi hizo, na zaidi ya nchi 50 zilikuwa zimeka mikakati ya kitaifa ya utekelezaji ya kushughulikia methani au zilikuwa katika harakati za kufanya hivyo. Muungano wa Hali ya Hewa na Hewa Safi (CCAC) ulianzisha mikakati ya kitaifa ili kuunga mkono ahadi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuisaidia Nigeria kuweka lengo la kupunguza methani inayotokana na mafuta na gesi kwa asilimia 60 kufikia mwaka wa 2030.
Katika Kongamano la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi, IMEO ilizindua Mfumo wake wa Tahadhari na Kushughulikia Methani, mfumo mpya unaotegemea satelaiti wa kubainisha uzalishaji wa gesi inayoongeza joto hewani, hali inayoweza kuwezesha serikali na mashirika ya biashara kuishughulikia kwa wakati unaofaa. Kwa kuongezea, zaidi ya kampuni 80 za mafuta na gesi zimejitolea kupima na kupunguza uzalishaji wao wa methani kupitia Ubia wa Mafuta na Gesi ya Methani 2.0, kipengele muhimu cha mbinu inayoendeshwa na data ya IMEO.
