19 Sep 2019

Mradi wa China wa Msitu wa 'Ant Forest' washinda tuzo la Mabingwa wa Dunia linatolewa na Umoja wa Mataifa.

 

  • 'Ant Forest', imepokea tuzo kuu la mazingira linatolewa na Umoja wa Mataifa katika kitengo cha motisha na kuchukua hatua
  • 'Ant Forest' walituzwa kwa kuwahimiza watumizi wa bidhaa kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa, hali iliyopelekea mradi mkubwa wa upandaji wa miti na sekta ya kibinafsi nchini China.

 

 

Septemba 19,  2019 -- 'Ant Forest', Mradi unaohimiza kutochafua mazingira, umeshinda tuzo la mwaka wa 2019 la Mabingwa wa Dunia. Tuzo hili la kiwango cha juu la mazingira linatolewa na Umoja wa Mataifa kutokana na juhudi zilizowezesha watu nusu bilioni walio na nia nzuri ya kupunguza hewa ya ukaa kupanda miti katika baadhi ya maeneo kame zaidi Uchina. 

 

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa linatuza 'Ant Forest' katika kitengo cha 'Motisha na Kuchukua Hatua'.

 

Mradi uliozinduliwa na 'Ant Financial Services Group' hupendekeza matumizi ya nishati isiyochafua mazingira kwa kuwashawishi watumiaji wa bidhaa kupunguza hewa ya ukaa huku wanapoendelea na shughuli zao za kila siku ili kuyatunza mazingira. 

 

Watumizi wa 'Ant Forest' wanashauriwa kupunguza hewa ya ukaa kupitia shughuli zao za kila siku kama vile kutumia magari ya umma wanaposafiri na kulipia huduma mtandaoni. Kila wanapofanya hivyo, wanatuzwa alama za ‘green energy’ na zinapofikia idadi fulani, mti halisi hupandwa. Watumizi wanaweza kuona picha za miti yao kupitia setilaiti. Mbali na upandaji wa miti, watumizi wanaweza kuamua kutunza sehemu ya kipande cha ardhi kwenye jukwaa la 'Ant Forest', ambalo pia linatafuta kutumia ubunifu kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya watu wanaokaa maeneo ya karibu na misitu hiyo kwa kutumia teknolojia ya kidijitali. 

 

Tangu kuzinduliwa kwake mnamo Agosti mwaka wa 2016, 'Ant Forest' na wabia kutoka katika mashirika yasiyokuwa ya serikali  (NGO), wamepanda takribani miti milioni 122 katika baadhi ya maeneo kame zaidi Uchina, ikiwa ni pamoja na maeneo kame ya Inner Mongolia, Gansu, Qinghai and Shanxi. Miti hiyo inapatikana katika eneo la hekta 112,000 (mu milioni 1.68);  Mradi huu ndio mkubwa sana Uchina wa upandaji wa miti unaofanywa na sekta za kibinafsi. 

 

"'Ant Forest'" ni idhibati ya jinsi teknolojia inavyoweza kubadili ulimwengu wetu kwa kutumia nishati nzuri na kuonyesha ubunifu wa watumizi kote ulimwenguni," alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa. 

 

“Ijapokuwa kuna changamoto kubwa zinazokabili mazingira, tuna teknolojia na maarifa ya kuzikabili na kubadili jinsi tunavyoishi katika sayari. Miradi kama  ya 'Ant Forest' ni mojawapo ya jinsi mwanadamu anavyoweza kutumia uerevu na ubunifu kuboresha maisha," alisema.

 

Haja ya kuchukua hatua kali kote ulimwenguli ili kukabiliana ya mabadiliko ya tabianchi itaangaziwa wakati wa Mkutano Mkuu wa Kushughulikia Mazingira ulioandaliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres’, utakaofanyika tarehe 23 Septemba mjini New York. Katibu Mkuu ametoa wito kwa viongozi duniani, wamiliki wa biashara na mashirika ya uraia kuhudhuria mkutano wakiwa na suluhisho tosha la jinsi watakavyopunguza uchafuzi wa hewa kwa asilimia 45 kufikia karne ijayo na kuepukana na hewa chafu kabisa kufikia mwaka wa 2050. Hii ni sambamba na Mkataba wa Paris kuhusu  tabianchi na Malengo ya Maendeleo Endelevu.  

 

Mkutano huu unalenga kutoa masuluhiho ya kipekee katika sekta za kipekee: kuhimiza matumizi ya nishati jadidifu duniani; miundo mbinu na miji endelevu na ya kudumu; mabadiliko ya kudumu ya  kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi; utengaji wa fedha na sekta za umma na za kibinafsi ili kuimarisha uchumi kwa kutochafua mazingira; na kilimo endelevu na utunzaji wa misitu na bahari.

 

Kutuzwa kwa 'Ant Forest' kama Bingwa wa Dunia inaonyesha umuhimu wa kutunza mifumo ya ekolojia ili kupunguza uzalishaji wa hewa inayosababisha mabadiliko ya tabianchi. Mnano Machi, Umoja wa Mataifa ulisisitiza umuhimu wa udharura wa kutunza mifumo inayowezesha maisha kwa kutangaza Karne ya kuanzia 2021 hadi 2030 kama karne ya Umoja wa Mataifa ya Kuboresha Mifumo ya Ekolojia. 

 

"Tuna furaha kubwa kupokea tuzo hili la Mabingwa wa Dunia," alisema Eric Jing, Mwenyekiti na Afisa Mkuu Mtendaji wa 'Ant Financial'. "'Alipay Ant Forest' ni ishara ya imani yetu kuwa teknolojia inaweza na ni sharti itumiwe kwa manufaa ya jamii. Tunashukuru watu wote wanaotumia teknolojia yetu na wabia ambao wametuwezesha kupanda miti milioni 122 na kukuza maono tunayoshiriki ya maendeleo endelevu ya kudumu. Kuvuma kwa 'Alipay Ant Forest' ni ishara kuwa umma uko tayari kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mabingwa wa Dunia, ni tuzo la kimataifa linalotolewa na Umoja wa Mataifa kwa heshima ya mazingira.  Lilianzishwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) mwaka wa 2005 kuwatuza watu wa kipekee ambao matendo yao yamekuwa na athari chanya zinazoleta mabadiliko kwa mazingira.  Kutoka kwa viongozi duniani hadi kwa watetezi wa mazingira na hadi kwa wanaobuni teknolojia, waanzilishi hawa wanaoleta mabadiliko ili kutunza sayari yetu kwa ajili ya vizazi vijavyo hutuzwa.  

 

'Ant Forest' ni mojawapo wa washindi tano wa mwaka huu. Vitengo vingine ni pamoja na Uongozi wa Sera , Maono ya Ujasiriamali  na Sayansi na Ubunifu. Washindi wa mwaka wa 2019 watatuzwa wakati wa sherehe ya gala mjini New York tarehe 26 Septemba wakati wa kikao cha 74 cha Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa.  Wengine watakaotuzwa pia wakati wa hafla hii ni wanamazingira wa kipekee saba wa umri wa kati ya miaka 18 hadi miaka 30. Watatuzwa tuzo la Vijana Bingwa Duniani.

 

Watu waliowahi kushinda tuzo la Mabingwa wa Dunia ni Wachina waliobuni vitu na waleta mabadiliko, hasa katika nyanja ya kukabiliana na uchafuzi wa mazigira na majangwa.  Katika mwaka wa 2018 programu ya 'Green Rural Revival Programme' ilituzwa katika kitengo cha motisha na kuchukua hatua kutokana na kazi yake ya kusafisha maeneo ya maji yaliyochafuliwa na kuboresha ardhi iliyoharibika. Katika mwaka wa 2017, Jamii ya Upandaji Miti ya Saihanba ilituzwa katika kitengo cha motisha na kuchukua hatua kwa kufanya ardhi iliyoharibika Kusini mwa Inner Mongolia kuzalisha mimea mingi.  

 

MAKALA KWA WAHARIRI

 

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa ni msemaji mkubwa wa kimataifa kuhusu mazingira. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika kutunza mazingira kupitia kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.   

 

Kuhusu Weibo

Mabingwa wa Dunia huandaliwa kwa msaada wa ufadhili kutoka kwa  Weibo – Mtandao mkuu wa kijamii nchini China unaowezesha watu kuunda, kushiriki na kupata makala mtandaoni.  Weibo ina zaidi ya watumizi milioni 486 kila mwezi.

 

Kuhusu Mabingwa wa Dunia

Tuzo linalotelewa kila mwaka la Mabingwa wa Dunia  hutuza viongozi vya kipekee kutoka kwa serikali, mashirika ya uraia na sekta ya kibinafsi ambao matendo yao yamesababisha mabadiliko chanya kwa mazingira. Tangu mwaka wa 2005, tuzo la Mabingwa wa Dunia limewatuza washindi 88, kuanzia kwa wakuu wa nchi hadi kwa wanaobuni teknolojia.  

 

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Keisha Rukikaire, UNEP Habari na Vyombo vya Habari, rukikaire@un.org, +254 722 677747

Related