Pixabay
19 May 2021 Toleo la habari Nature Action

Dunia imefikia malengo ya maeneo yaliyolindwa kwenye ardhi, ila ubora wake unahitaji kuimarishwa

Ripoti ya UNEP/IUCN ya Sayari Iliyolindwa: maendeleo makubwa tangu mwaka wa 2010 kukiwa na zaidi ya kilomita mraba milioni 22 ya ardhi na kilomita mraba milioni 28  iliyolindwa au kuhifadhiwa na asilimia 42 ya idadi hii ikiongezwa katika muongo uliopita; na ardhi isiyozidi asilimia 8 imelindwa na kuunganishwa.

Nairobi, Mei 19, 2021 - Jamii ya kimataifa imepiga hatua kubwa ya kufikia malengo ya kimataifa kuhusiana na maeneo yaliyolindwa na kuhifadhiwa, ilahaijafikia malengo yake kuhusu ubora wa maeneo haya, kwa mjibu wa ripoti mpya kutoka kwa Kituo cha Ufuatiliaji wa Uhifadhi Duniani cha Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP-WCMC) na Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira(IUCN), ilitolewa kwa ushirikiano na Shirika la Jiografia ya Kitaifa.

Toleo la hivi karibuni linalotolewa kila baada ya miaka miwili la Ripoti ya Sayari Iliyolindwa Ripoti ya Sayari Iliyolindwa inaonyesha matokeo ya mwisho ya Aichi Target 11 – malengo ya kimataifa ya miaka 10 kuhusiana na maeneo yaliyolindwa na kuhifadhiwa yaliyolenga kuzalisha manufaa makubwa kwa bayoanuai na watu kufikia mwaka wa 2020. Aichi Target 11 ilijumuisha malengo ya kulinda angalau asilimia 17 ya ardhi na maji yanayopatikana kwenye maeneo ya ardhi na asilimia 10 ya mazingira ya baharini. Kwa sasa, kilomita mraba milioni 22.5 (asilimia 16.64) ya mifumo ya ekolojia ya ardhi na maji yanayopatikana kwenye maeneo ya ardhi na kilomita mraba milioni 28.1 (asilimia 7.74) ya maji ya maeneo ya pwani na bahari vimejumuishwa kwenye maeneo yaliyolindwa na kuhifadhiwa, ongezeko la zaidi ya kilomita mraba milioni 21 (asilimia 42 ya hali halisi) tangu mwaka wa 2010, yaonyesha ripoti mpya. Ni dhahiri kuwa maeneo ya ardhi itazidi mno lengo la asilimia17 lililowekwa iwapo data ya maeneo yote itakusanywa, kwa sababu taarifa kuhusu maeneo mengi yaliyolindwa hazijatolewa.

Mpango wa bayoanuai duniani baada ya 2020 utaafikiwa kwenye Kongamano la Bayoanuai la Umoja wa Mataifa (CBD COP15) mjini Kunming, nchini China, mwezi wa Octoba na inatarajiwa kujumuisha ahadi za kuimarisha ubora wa maeneo yaliyolindwa na kuhifadhiwa. Ripoti ya Sayari Iliyolindwa inadokeza kuwa kutakuwa na changamoto ya kuimarisha ubora wa maeneo yaliyopo na maeneo mapya ili kupata mabadiliko chanya kwa watu na mazingira, kwa sababu bayoanuai inaendelea kudidimia hata kwenye maeneo mengi yaliyolindwa. IUCN Green List Standard ndiyo pekee hutumika kote duniani kukadiria ubora wa mabadiliko.

Neville Ash, Mkurugenzi, UNEP-WCMC anasema: "Maeneo yaliyolindwa na kuhifadhiwa ni muhimu katika kukabiliana na uharibifu wa mifumo ya ekolojia, na hatua kubwa zimepigwa katika miaka ya hivi karibuni za kuimarisha mitandao ya kimataifa ya maeneo yaliyolindwa na kuhifadhiwa. Hata hivyo kuchagua na kuwajibikia haitoshi; yanahitaji kusimamiwa vyema na kushughulikiwa kwa usawa ili kujipatia manufaa mengi katika ngazi ya eneo na ya kimataifa na kuwa na mustakabali bora  kwa watu na sayari. ”

Ufanisi na usawa ni muhimu baada ya 2020

Ili kufanikiwa, maeneo yaliyolindwa na kuhifadhiwa yanahitaji kujumuisha maeneo muhimu kwa bayoanuai. Walakini, theluthi moja ya maeneo muhimu ya bayoanuai, iwe ni juu ya ardhi, maeneo ya maji kwenye ardhi au bahari, bado hayajalindwa hata kidogo, kulingana na ripoti hiyo.

Maeneo yaliyolindwa na yaliyohifadhiwa pia yanahitaji kuunganishwa vizuri, ili kuruhusu spishi kuzunguka na michakato ya ekolojia kufanya kazi. Ingawa kumekuwa na kuimarika hivi karibuni, chini ya asilimia 8 ya ardhi zote zimelindwa na kuunganishwa - kidogo kabisa ikilinganishwa na takribani asilimia 17 ya eneo la ardhi ambalo sasa linalindwa - na bado kuna haja ya kuhakikisha maeneo yalio karibu yanasimamiwa ipasavyo kudumisha maadili ya bayoanuai.

Pamoja na kuteua maeneo mapya, ripoti hiyo inataka maeneo yaliyolindwa na kuhifadhiwa kuainishwa na kutambuliwa, kwa kuwajibikia juhudi za watu wa kiasili, jamii za wenyeji na mashirika ya kibinafsi, huku tukitambua haki na wajibu wao. Jitihada za uhifadhi wa walinzi hawa bado hazijathaminiwa na zimeripotiwa kidogo, ingawa michango yao ni mikubwa kwa hatima ya mazingira.

Ripoti hii pia inaonyesha kuwa juhudi zaidi zinahitajika kusimamia maeneo yaliyolindwa na kuhifadhiwa kwa usawa, ili gharama za uhifadhi zisibebwe na watu wa eneo hilo wakati faida zake zinafurahiwa na wengine. Hii ni muhimu ili kujenga mitandao ya uhifadhi ambayo inaungwa mkono na kujumuisha watu kila mahali.

“IUCN inakumbatia maendeleo makubwa yaliyopatikana, hasa katika muongo mmoja uliopita, huku maeneo yaliyohifadhiwa yakiongezeka ulimwenguni. Bayoanuai inapoendelea kudidimia, tunatoa wito kwa watakaoshiriki kwenye Kongamano la Bayoanuai la Umoja wa Mataifa mjini Kunming kuweka malengo kabambe yatakayohakikisha kuwa asilimia 30 ya ardhi, maji safi na bahari inalindwa kufikia mwaka wa 2030. Haya ni sharti yazingatiwe ili kulinda uanuai wa maisha duniani na kusimamiwa kwa njia mwafaka na kwa usawa,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa IUCN Dkt Bruno Oberle.

Kutunza na kuboresha mazingira ni mambo yanayotegemeana

Kwa kulinda maeneo ambayo hayajaharibika na kuboresha mifumo ya ekolojia iliyoharibika, nchi zinaweza kuunda mtandao wa mazingira utakaosaidia kukomesha na kukabiliana na uharibifu wa bayoanuai, kudumisha huduma muhimu za mifumo ya ekolojia, kusaidia jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza hatari za magonjwa tandavu baadaye. Sehemu zinazosimamiwa vyema, zilizolindwa na kuhifadhiwa zinaweza kusaidia kuzuia uharibifu zaidi wa mifumo ya ekolojia na kuimarisha maendeleo kwenye Muongo wa UN wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia. Muongo utazinduliwa rasmi tarehe 5 Juni, Siku ya Mazingira Duniani mwaka wa 2021. Mara nyingi, maeneo yanayoboreshwa yataweza kuongezwa kwenye mtandao wa eneo linalolindwa na kuhifadhiwa moja kwa moja, ili kuhakikisha kuwa manufaa ya uboreshaji yanadumishwa.

MAKALA KWA WAHARIRI

Ripoti kamili inapatikana kwa vyombo vya habari kupitia http://livereport.new-web.pp-staging.linode.protectedplanet.net/

Ikiruhusiwa kuchapishwa (tafadhali kumbuka tovuti inayopatikana sasa kupitia kiunga hiki ni Ripoti ya Sayari Iliyolindwa ya mwaka wa 2018. Ripoti mpya itaweka itaweka wakati wa uzinduzi): https://livereport.protectedplanet.net/    

Waandishi wa ripoti wanapatikana kwa mahojiano.

Pia watashiriki kwenye uzinduzi wake mtandaoni: Jumatano Mei 19, 10:15am US ET / 14:15 GMT / 15:15 BST / 16:15 CET

Kujiunga: https://zoom.us/webinar/register/WN_LAHleGkGTUyqVYsawtJBhw

Kuhusu UNEP-WCMC

Kituo cha Ufuatiliaji wa Uhifadhi Duniani cha Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP-WCMC) ni kituo kikuu kinachoshughulikia bayoanuai, kinachoshirikiana na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa na shirika la msaada la WCMC. UNEP-WCMC hutumia sayansi, sera, na mazoeza kusaidia kukabiliana na changamoto za mazingira ulimwenguni.

Kuhusu IUCN

IUCN ni muungano wa wanachama kutoka kwa serikali na mashirika ya uraia. Inashirikisha uzoefu, rasilimali na ufikiaji wa Wanachama wake walio zaidi ya mashirika 1,400 na mchango kutoka kwa wataalam zaidi ya 18,000. IUCN ni mamlaka ya kimataifa kuhusu hali ya mazingira asilia ulimwenguni na hatua zinazohitajika kuyalinda.

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP):

UNEP in mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira ulimwenguni. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.    

Kuhusu Muongo wa UN wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia

Ikiongozwa na UNEP na Shirika la Chakula na Kilimo, Muongo wa UN utapata msaada wa kisiasa, utafiti wa kisayansi na fedha ili kuimarisha uboreshaji wa mifumo ye ekolojia kwa lengo la kufufua mamilioni ya hekta za mifumo ya ekolojia ya ardhini na majini.

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Haf Davies, Msimazi wa Vyombo vya Habari na Kidiijitali, UNEP-WCMC, +447952 920 159, haf.davies@unep-wcmc.org
Goska Bonnaveira, Meneja wa Vyombo vya Habari na Mawasiliano, IUCN, +41 79 276 01 85, Goska.Bonnaveira@iucn.org

Keishamaza Rukikaire, , Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, UNEP,