Pixabay/Accessed 24 Jan 2022
24 Jan 2022 Toleo la habari Youth, education & environment

UNEP yazindua zana mpya zisizolipishwa za kufundisha kuhusu tambiko la ozoni na utunzaji wa mazingira

  • Zana mpya za walimu mtandaoni zisizolipishwa na mpangilio wa masomo kutokana na mafanikio ya Reset Earth, uhuishaji na mchezo wa video wa Sekretarieti ya Ozoni ya UNEP.
  • Zinalenga Vijana kwa kutumia uhuishaji na apu kuunda masomo ya mtandaoni kwa ubunifu ili kuhamasisha kuhusu tabaka la ozoni na utunzaji wa mazingira.
  • Zinapatikana mtandaoni kwenye muundo wa kidijitali na unaoweza kuchapishwa ili  kufikiwa na wote

 

Nairobi, Kenya, Januari 24, 2022 - Ili kuunga mkono Siku ya Elimu Duniani na walimu wanaotafuta nyenzo mpya kuhusu uhamasishaji na utunzaji wa mazingira, Sekretarieti ya Ozoni ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa imejihusisha na uhuishaji na matumizi ya apu kuunda mpangilio wa masomo kwa njia bunifu wa kutumiwa na walimu na vitabu vya mazoezi kwa wanafunzi. 

Zinalenga vijana (wenye umri kati ya miaka 8 na 12) na kwa kutumia uhuishaji na hadithi fupi za Reset Earth, wahusika wakuu Knox, Terran na Sagan wanasimulia kuhusu tambiko la ozoni lilivyookolewa. Zana hizi zinapatikana mtandaoni bila malipo kwenye jukwaa la elimu la Sekretarieti ya Ozoni. Zikiwa zimeundwa mahususi kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya nyenzo bora na bunifu za kujifunzia mtandaoni, zana hizo pia zinaweza kuchapishwa na vipindi vinapatikana katika umbo la futuhi ili kufikia watu wote.

Awamu ya kwanza ya zana hizo inalenga kutoa utangulizi kukusu sayansi ya mazingira ili kusaidia kuelimisha, kuhamasisha na kuchochea hatua miongoni mwa vijana kuhusu umuhimu wa tabaka la ozoni, na hitaji la kudumu la kulitunza. Awamu ya Pili, inayolenga vijana, inaendelea kufanyiwa kazi na itazinduliwa hivi karibuni. 

“Siwezi kusisitiza umuhimu wa kuendelea kutunza tabaka la ozoni na hadithi ya Protokali ya Montreal wakati huu wa changamoto kuu ya mabadiliko ya taianchi," Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Ozoni, Meg Seki alisema. “Ni hadithi ya matumaini kwa kizazi chetu cha vijana.  Pia ni ukumbusho kwetu sote kujitahidi kuwa na ushirikiano wa kimataifa na ubia ili kuunda na kutekeleza sera za kimataifa za mazingira zinazozingatia sayansi.”

Tambiko la ozoni ni kinga isiyoonekana iliyoko kati ya kilomita 15 na 35 kwenye eneo la anga la juu zaidi kutoka Duniani, linalolinda wanadamu, wanyama, mimea na mifumo muhimu ya ekolojia dhidi ya mionzi hatari ya UV.

Katika miaka ya 1980, wanasayansi waligundua shimo kubwa kwenye tabaka la ozoni, lililosababishwa na utoaji wa klorofluorokaboni (CFC). Kemikali hii iliyotengenezwa na mwanadamu ilitumika kwenye bidhaa nyingi - mikebe ya erosoli, friji, viyoyozi, sponji za kupunguza joto, vizima moto, viyeyusho na bidhaa nyingine nyingi.

Wakionywa na wanasayansi, viongozi wa dunia na watungasera walishirikiana, na kuchukua hatua za dharura kudhibiti na kukomesha CFCs na vitu vingine vinavyoharibu ozoni duniani kote.  Protokali ya Montreal kuhusu Bidhaa Zinazoharibu Tabaka la Ozoni ilipitishwa mwaka wa 1987.  Tangu wakati huo, imeidhinishwa kote ulimwenguni na mataifa 197 na Muungano wa Ulaya, na kuifanya kuwa mojawapo ya mikataba yenye mafanikio zaidi ya mazingira.  Kukomesha vitu vinavyoharibu ozoni pia kumechangia pakubwa kupunguza mabadiliko ya tabianchi kwa sababu vitu hivyo huzalisha mno gesi hatari mno ya ukaa.   

Lakini kuboresha tambiko la ozoni iliyoharibiwa na kulirejeshea hali yake ya viwango vya kabla ya mwaka wa 1980 kutachukua miongo kadhaa.  Itahitaji kujitolea kwa mara kwa mara na utunzaji utakaofanywa na jamii ya Protokali ya Montreal na vizazi vijavyo.  Changamoto za mazingira ambazo kizazi kijacho cha vijana kinakabiliwa nazo ni nyingi.  Lakini hadithi ya tabaka la ozoni na ushirikiano wa kimataifa kulitunza, ni hadithi ya matumaini.  Protokali ya Montreal ni ukumbusho kwamba wakati ulimwengu unapokuja pamoja na kushirikiana, kwa kuongozwa na sayansi, wanadamu wanaweza kutatua changamoto kubwa mno duniani.

Makala kwa Wahariri

Sekretarieti ya Ozoni ya Umoja wa Mataifa

Sekretarieti ya Ozoni iko mjini Nairobi, nchini Kenya, chini ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP). Ni Sekretarieti ya mikataba/makubaliano mawili muhimu sana ya utunzaji wa ozoni: Mkataba wa Vienna wa Kutunza Tabaka la Ozoni na Protokali ya Montreal kuhusu Vitu Vinavyoharibu Tabaka la Ozoni.  Yote mbili ina wajibu mkubwa wa kutunza tabaka la ozoni na kupunguza uharibifu wake.  Dhamira ya Sekretarieti ni kuwezesha utekelezaji mzuri wa Mkataba wa Vienna na Protokali ya Montreal na marekebisho yaliyofanywa.

Kuhusu Maadhimisho ya Miaka 50 ya UNEP

Kongamano la Umoja wa Mataifa la mwaka wa 1972 kuhusu Mazingira ya Binadamu mjini Stockholm, Uswidi, lilikuwa la mwanzo kuwahi kutumia neno "mazingira" kwenye anuani yake.  Kuanzishwa kwa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) ni mojawapo ya matokeo yanayodhihirika ya Kongamano hili la kipekee.  UNEP ilianzishwa kama kitengo cha UN cha kushughulikia mazingira duniani.  Shughuli zinazoendelea mwaka mzima wa 2022 zitaangazia mafanikio makuu yaliyofikiwa na yale yanayotarajiwa kutokea katika miongo ijayo.

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani.  Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.

Kwa mawasiliano zaidi, tafadhali wasiliana na:

Stephanie Haysmith, Afisa wa mawasiliano, Sekretarieti ya Ozoni