15 Jul 2019 Toleo la habari Malengo ya Maendeleo Endelevu

Vijana wazingatia mafundisho ya kidini kuikoa sayari

Julai 15, 2019 – Jinsi suala a kushughulikia mazingira linapoendelea kupata umaarufu kote ulimwenguni, viongozi ambao ni vijana wapatao 350 kutoka katika zaidi ya nchi 50 leo walijadili masuluhisho, wakatathmini mifano ya kibunifu na mazoea bora wakati walipokutana katika kongamano la pili la kimataifa la kati ya dini mbalimbali la Laudato Si’ (the second international Laudato Si’ interfaith conference) lililofanyika katika Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa lenye makao yake makuu mjini Nairobi.

Washiriki, haswa vijana ambao ni viongozi wa kidini walijumuisha wabia wa kidini kutoka kwa dini mbalimbali, watu kutoka kwa jamii asili na mashirika ya mazingira, waliokutana chini ya mada, Laudato Si' generation: Young people caring for our common home.

"Nina matumaini kwa vijana wa kike na wa kiume kote ulimwenguni ambao wanatumia dini pamoja na sayansi kufanya kampeni za kuleta mabadiliko na kufanya uhamasishaji wa jinsi ya kuwa na maisha endelevu," alisema Joyce Msuya, Naibu wa Mkuu wa UNEP.

"Sisi katika Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa tunafanya kazi kwa bidii kila siku ili kujiandaa kwa siku za baadaye endelevu. "Tumejitolea kwa dhati kufanya kazi na vijana, pamoja na viongozi wa dini na mashirika ya kidini kutoka pembe zote ulimwenguni, ili kufikia malengo yaliyowekwa katika Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu."

Miaka minne iliyopita, katika Waraka wa Baba Mtakatifu, Laudato Si’, Papa Francis alisisitiza umuhimu wa kuwaza kuhusu udhaifu wa ulimwengu na mamilioni ya watu maskini wanaoteseka sana kutokana na maendeleo yanayofanywa na binadamu yanayoharibu mazingira. Alisema ni muhimu kufanya maamuzi ya kibinafsi yaliyo na manufaa badala ya kutaka kufanya matamanio yetu ya mda mfupi.

"Kama ilivyoanishwa katika Laudato Si’, janga la kiekolojia tunalokumbana nalo ni tata na linajitokeza kwa namna mbalimbali," alisema Kadinali Peter Turkson, Kiranja wa Idara katika Afisi ya Papa ya Kukuza Maendeleo Muhimu kwa Binadamu (Dicastery for Promoting Integral Human Development), katika ujumbe uliosomwa na Kasisi (His Excellency Mgr.) Bruno-Marie Duffé, Katibu wa Idara katika Afisi ya Papa ya Kukuza Maendeleo Muhimu kwa Binadamu.

"Kanisa limejitolea kutekeleza wajibu wake wa kuhamasisha na kutoa wito wa kuchukua hatua, huku wakishirikiana na wanakijiji wanaendelea kung'ang'ana nyanjani," aliongezea.

"Akielezea yaliyojiri wakati wa kimbunga cha Cyclone Idai – kilichosababisha maafa makubwa wakati kilikumba sehemu za Msumbiji, Zimbabwe, na Malawi mwezi wa Machi – Jessica Gimo mwenye umri wa miaka 25 kutoka Beira, Mozambique, alisema kuwa kuna uwezekano wa kupunguza madhara na kuzuia majanga yatokanayo na hali ya hewa iwapo tutakuwa na taarifa za kutosha.

"Kwa mtazamo wangu, Ukosefu wa taarifa ulizidisha madhara, kwa sababu iwapo wangetufahamisha kuhusu ukubwa wa kimbuga cha Cyclone Idai, tungefanya mpango wa kuhamia kwa miji salama. Ninaamini ya kuwa hali ingekuwa tofauti na pengine madhara yangekuwa machache," alisema.

Katika mwaka wa 2017, UNEP ilizindua mradi wa Faith for Earth initiative, ambao tayari umejiundia mtandao wa washiriki zaidi ya 750 kutoka kwa mashirika ya kidini ili kunufaisha sayari kutokana na nguvu za dini. Mwaka uo huo mradi wa Interfaith Rainforest Initiative, ulianzishwa kwa nia ya kuzua udharura wa kimaadili na uongozi wenye misingi ya kidini ili kukomesha uharibifu wa misitu yetu ya kitropiki.

Wakati wa kongamano, Mradi wa Imani kwa ajili ya Dunia (Faith for Earth Initiative) wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa - kwa ushirikiano wa wabia wanaojumuisha Mtandao wa Vijana wa Kikatoliki kwa Mazingira Endelevu AfrikaCYNESA), Afisi ya Mfuko wa Wanyama Pori Duniani wa Afisi ya Eneo la Afrika,  Young Muslim Association na Dicastery for Promoting Integral Human Development – waliwasikiliza wazungumzaji walitoa mwelekeo wa kisayansi kuhusu hali ya sasa ya dunia na wakajadili umuhimu wa vijana kuhusika.

Kongamano la Laudato Si conference hutokea kwa wakati mmoja na Siku ya Ujuzi wa Vijana Duniani, na hutokea siku kadhaa baada ya mitandao inayowakilisha zaidi ya vyuo na taasisi za masomo ya ngazi za juu 7,000 kutoka kwa mabara 6 zilipotangaza kuwazinatangaza Udharura wa Kushughulikia Tabia nchi, na pia walikubali kutumia mpango wenye vipengele vitatu kushughulikia janga hilo kupitia kazi yao wakishirikiana na wanafunzi.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP ni msemaji mkubwa wa kimataifa kuhusu mazingira.   Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika kutunza mazingira kupitia kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.   UNEP hufanya kazi pamoja na serikali, sekta ya kibinafsi, mashirika ya uraia na Taasis zinginezo za Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa kote ulimwenguni.

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Kitengo cha Habari na Media, unenvironment-newsdesk@un.org