20 Jan 2020 Tukio Miji

Ushauri mkuu kuhusu jinsi ya kushinda: Kijana Bingwa Duniani kutoka eneo la Asia na Pasifiki

Jukwaa la Sonika Manandhar la 'Green Energy Mobility'  linaleta suluhu  kutokana na data kubwa na liliundwa na  Kijana Bingwa Duniani wa mwaka wa 2019 kutoka eneo la Asia na Pasifiki ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi nchini Nepal.

Maono yake ni kuwasaidia wanawake kumiliki na kutumia Safa Tempos—magari ya miguu mitatu yanayotumia nguvu za umeme na yanayopatikana kupitia mkopo unaolipisha riba kidogo. Jukwaa hili linanuia kuwezesha kuwepo na magari ya umma yanayotumia nguvu za umeme badala ya matumizi ya magari ya kibnafsi, hasa kwa wanawake ambao ni hatari kwao kufanya kazi usiku katika eneo la Kathmandu na katika maeneo mengine.

Bert Fabian, Afisa wa Kitengo cha Ubora na Mzunguko wa Hewa cha Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, alisema: "Mfumo uliopo wa usafiri unategemea mno nishati ya visukuku ila hali hii inapaswa kusitishwa.

"Wakiongoza kupitia kwa matendo yao, vijana kama Sonika wanafanya juhudi za kuhakikisha kuna matumizi ya nishati isiyochafua mazingira. Lengo lake la  kuwezesha kuwa na usafiri kwa kutumia magari ya umeme na kuwawezesha wanawake kwa wakati mmoja ni jambo la kutia moyo, na mambo kama haya yanapaswa kuimarishwa na kurudufishwa kote duniani ili kuleta mageuzi halisi."

Tulimwuliza Manandhari kutoa ushauri mkuu wa jinsi ya kushinda tuzo hili. Iwapo una umri wa kati ya miaka 18 na 30 na wazo linalohusiana na masuala ya mazingira, mbona usishiriki?

Hongera kwa kushinda tuzo la Vijana Bingwa Duniani! Una mawaidha yepi kwa wale wangependa kushiriki katika mwaka wa wa 2020?

Kama mhandisi, ningependa kuwashauri wahandisi wenzangu wasizame katika masuala ya kiufundi mno. Unapozungumzia matatazo ya kijamii na matatizo ya mazingira si vyema kutafuta suluhu kwa njia ya kiufundi. Tatua kwa njia inayoeleweka kwa wote. Suala hili lilinisumbu kwa mda, kwa hivyo ni vyema kuliweka wazi hasa kwa wale ambao wangependa kushiriki.

Je, ulikuwa na tajriba ipi wakati ulituma ombi la kushiriki?

Kabla ya kutuma ombi, ni vyema kutafakari kuhusu jinsi suluhisho lako litakavyofanya kazi. Fanya utafiti mwanzo na ikiwezekana ufanye utafiti wa jaribio nyanjani, ili kukusanya data fulani. Usihofie yatakayotokea. Unaingia kwenye jukwaa la kimataifa na utapaswa kueleza kuhusu yale ambayo umeweza kufanya hadi sasa na vile unavyoweza kufaulu. Kwa hivyo ninadhani ni vyema kuwa na uzoevu fulani na wala sio tu kuwa na wazo wakati wa kushindana.

Iwapo utapewa fursa ya kutoa ushauri kwa wenzako, utawaambia nini?

Fanya unayoweza! Usiogope. Pitia ombi lako na mtu unayemwamini, ili wakupe maoni yao kuhusu jinsi anbavyo umetoa ombi lako. Lakini wasiwe watu wengi kwa sababu mwishowe watakukanganya! Jiamini mwenyewe na uamini wazo lako.

Je unaamini kuwa waweza kuwa Kijana Bingwa Duniani? Wito utatolewa mwanzoni mwa mwaka wa 2020. Unapotuma ombi la kushiriki, unajiunga pia na jamii ya waleta mabadiliko. Tufuatilie!

Tuzo la Vijana Bingwa Duniani, linalodhaminiwa na Covestro, ni mradi mkuu wa  Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa unaowashirikisha vijana kukabiliana na changamoto kuu za mazingira ulimwenguni.