Miranda Grant, UNEP
02 Nov 2023 Toleo la habari Kushughulikia Mazingira

Kadiri athari za mabadiliko ya tabianchi zinavyoongezeka, pengo la ufadhili wa Kukabiliana na Pengo la Juhudi za Kukabiliana na Uzalishaji…

  • Mahitaji ya kifedha ya nchi zinazoendelea sasa ni kati ya mara 10 na 18 zaidi kwa kuzingatia mtiririko wa kimataifa wa fedha za umma
  • Kuongezeka kwa pengo kunatokana na kupanda kwa mahitaji ya kukabiliana na hali na kupungua kwa fedha za kukabiliana na hali hii
  • Kushindwa kuimarisha ukabilianaji wa hali kuna athari kubwa kwa hasara na uharibifu 

Nairobi, Novemba 2, 2023 – Hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinapungua katika kila nyanja wakati ziinapopaswa kuongezeka ili kukabiliana na athari na madhara ya mabadiliko ya tabianchi, kulingana na ripoti mpya ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).

Inayotolewa kabla ya mkutano wa mazingira wa COP28 mjini Dubai, Miliki za Falme za nchi za Kiarabu, Ripoti ya Kukabiliana na Pengo la Juhudi za Kukabiliana na Uzalishaji Wa Gesi Chafu mwaka wa 2023 Hakuna ufadhili wa kutosha, wala maandalizi ya kutosha– Uwekezaji duni na mikakati duni ya kukabiliana na  mabadiliko ya tabianchi ni hatari kwa dunia inaonyesha kuwa mahitaji ya kifedha ya nchi zinazoendelea sasa ni kati ya mara 10 na 18 zaidi kwa kuzingatia mtiririko wa kimataifa wa fedha za umma – asilimia 50 zaidi kuliko makadirio ya hapo awali.

"Ripoti ya Leo ya Pengo la Juhudi za Kukabiliana na Uzalishaji Wa Gesi Chafu inaonyesha kuongezeka kwa pengo kati ya mahitaji na hatua kuhusiana na suala la kulinda watu dhidi ya majanga yanyayotokana na tabianchi. Juhudi za kulinda watu na mazingira ni muhimu zaidi sasa kuliko hapo awali," Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema katika ujumbe wake kuhusu ripoti hii. "Maisha na njia za kujipatia riziki zinapotea na kuharibiwa, huku walio hatarini wakiteseka zaidi."

"Tunapaswa kukabiliana na hali hii kwa dharura. Ni lazima tuchukue hatua kuzingatia hali iliopo. Na tuchukue hatua za kuziba pengo la kukabiliana na hali hii, sasa," aliongeza.

Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya kifedha ya kukabiliana na pengo la ufadhili wa juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa sasa linakadiriwa kuwa dola za Marekani bilioni kati 194 na 366 kwa mwaka. Wakati uo huo, mikakati na utekelezaji wa juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi inaonekana kuwa mibovu. Kushindwa huku kukabiliana na hali kuna athari kubwa kwa hasara na uharibifu, haswa kwa walio hatarini zaidi.     

“Katika mwaka wa 2023, mabadiliko ya tabianchi bado yalikuwa na usumbufu zaidi na mabaya zaidi: joto liliongezeka na kuvunja rekodi, huku dhoruba, mafuriko, mawimbi ya joto na mioto misituni vikisababisha uharibifu," Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP alisema. "Athari hizi zinazoongezeka zinatuambia kwamba dunia lazima ipunguze kwa dharura uzalishaji wa gesi ya ukaa na kuimarisha juhudi za kukabiliana na hali ili kulinda watu walio hatarini. Wala haya hayafanyiki.”

"Hata kama jamii ya kimataifa ingesitisha uzalishaji wa gesi za ukaa leo, uharibifu kutokana na mabadiliko ya tabianchi utachukua miongo kadhaa kutoweka," aliongezea. "Kwa hivyo, ninawasihi watungasera kuzingatia yaliomo katika Ripoti ya Kukabiliana na Pengo, kuimarisha ufadhili na kutumia COP28 kama wakati ambapo ulimwengu utajitolea kikamilifu kuhami nchi za kipato cha chini na makundi yaliyohatarini dhidi ya athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi."

 

Ufadhili, mikakati na utekelezaji duni

Baada ya sasisho kuu kuhusu miaka iliyopita, ripoti hii sasa inaonyesha kuwa fedha zinazohitajika kukabiliana na hali katika nchi zinazoendelea ni nyingi zaidi - zinakadiriwa kuwa dola za Marekani kati ya bilioni 215 na bilioni 387 kwa mwaka katika muongo huu.

Gharama za miradi ya kukabiliana na hali hiyo katika nchi zinazoendelea zinakadiriwa kuwa dola za Marekani bilioni 215 kwa mwaka katika muongo huu na zinatarajiwa kupanda kwa kiasi kikubwa kufikia mwaka wa 2050. Fedha za kukabiliana na hali hii zinazohitajika ili kutekeleza vipaumbele vya kukabiliana na hali hiyo, kwa kuzingatia uongezaji wa Michango Inayoamuliwa na Taifa na Mipango ya Kitaifa ya Kukabiliana na hali katika nchi zote zinazoendelea, inakadiriwa kuwa dola za Marekani bilioni 387 kwa mwaka.   

Licha ya mahitaji haya, mtiririko wa fedha za kukabiliana na hali za mashirika ya kimataifa na baina ya nchi mbili kwa nchi zinazoendelea ulipungua kwa asilimia 15 hadi dola bilioni 21 katika mwaka wa 2021.  Hali hii inajiri licha ya ahadi zilizotolewa katika COP26 mjini Glasgow kuwasilisha karibu dola bilioni 40 kwa mwaka kama msaada wa kifedha wa kukabiliana na hali kufikia mwaka wa 2025, hali inayotisha.

Ingawa nchi tano kati ya sita zina angalau chombo kimoja cha kitaifa cha mikakati ya kukabiliana na hali, hatua za kufikia utekelezaji wa kimataifa kikamilifu zinapungua.  Idadi na kiwango cha hatua za kukabiliana na hali zinazoungwa mkono kupitia ufadhili wa mazingira wa kimataif umeduwaa katika muongo uliopita.

 

 Njia bunifu za kupata ufadhili ni muhimu

Ukabilianaji wa hali kwa njia madhubuti unaweza kuimarisha ustahimilivu - ambayo ni muhimu sana kwa nchi za mapato ya chini na makundi yaliyo hatarini - na kumaliza hasara na uharibifu.

Ripoti hii inaelekeza kwenye utafiti unaoonyesha kuwa nchi 55 zenye uchumi unaoathiriwa zaidi na tabianchi pekee zimepata hasara na uharibifu wa zaidi ya dola za Marekani bilioni 500 katika miongo miwili iliyopita. Gharama hizi zitapanda kwa kasi katika miongo ijayo, hasa kwa kukosekana kwa mikakati kapambe ya kupunguza na kukabilianana hali.  

Utafiti unaonyesha kuwa kila bilioni iliyowekezwa katika kukabiliana na mafuriko katika maeneo ya pwani husababisha kupungua kwa gharama za kushughulikia uharibifu kwa dola za Marekani bilioni 14.  Wakati uo huo, dola bilioni 16 kwa mwaka zinazowekezwa katika kilimo zinaweza kuzuia takriban watu milioni 78 dhidi ya njaa au baa la njaa la kudumu kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Hata hivyo, lengo la mwaka wa 2019 la kuongeza maradufu ufadhili wa kimataifa kwa nchi zinazoendelea kufikia mwaka wa 2025 wala Lengo Jipya la Takwimu za  Pamoja kufikia mwaka wa 2030 havitaweza kuziba pengo la kifedha la kukabiliana na hali hiyo kivyake na kuzalisha matunda.

Ripoti hii inabainisha njia saba za kuimarisha ufadhili, ikiwemo kupitia matumizi ya ndani ya nchi na ufadhili wa kimataifa na wa sekta binafsi. Njia za ziada ni pamoja na utumaji fedha kama zawadi, kuongeza na kutoa ufadhili kwa Mashirika ya Biashara Madogo na ya Kati, utekelezaji wa Kifungu cha 2.1(c) cha Mkataba wa Paris kuhusu kubadilisha mtiririko wa fedha kuelekea njia za maendeleo zinazozalisha hewa ya ukaa kidogo na kustahimili mabadiliko ya tabianchi, na kufanyia mabadiliko mfumo wa ufadhili duniani kifedha wa kimataifa, kama ilivyopendekezwa na Mpango wa Bridgetown.  

Mfuko mpya wa kukabiliana na Hasara na Uharibifu pia utakuwa chombo muhimu cha kukusanya rasilimali, ila changamoto zitasalia kuwepo. Mfuko utahitaji kuzingatia mbinu bunifu zaidi za ufadhili ili kufikia kiwango kinachohitajika cha uwekezaji.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.  

 

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Kitengo cha Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa