Pixabay
03 Jun 2021 Toleo la habari Kutumia mazingira kushughulikia tabianchi

Umoja wa Mataifa watoa wito kwa nchi kutimiza ahadi za kupanda miti kwenye hekta bilioni moja ya ardhi

Juni 3, 2021, Nairobi/Roma – Kukabiliana na changamoto za aina tatu za mabadiliko ya tabianchi, bayoanuai, na uchafuzi, ulimwengu lazima utekeleze ahadi yake ya kupanda miti kwa maeneo iliyokatwa angalau kwa hekta bilioni moja za ardhi katika muongo mmoja ujao - eneo lililo karibu kutoshana na Uchina. Nchi pia zinahitaji kuongeza ahadi kama hizo kuhusu bahari, kulingana na ripoti mpya ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), mipango ya kuzinduliwa kwa Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia 2021-2030 inapoendelea.

Ripoti, #GenerationRestoration: Uboreshaji wa mifumo ya ekolojia kwa manufaa ya watu, mazingira na hali ya hewa, inasisitiza kuwa binadamu wanatumia angalau 1.6 zaidi ya huduma zinazoweza kutolewa na mazingira bila shinikizo. Hiyo inamaanisha juhudi za uhifadhi pekee hazitoshi kuzuia kudidimia kwa mifumo ya ekolojia na uharibifu wa bayoanuai kwa kiwango kikubwa. Gharama za kuboresha nchi kavu - bila kujumuisha gharama za kuboresha mifumo ya ekolojia ya baharini - inakadiriwa kuwa angalau dola bilioni 200 kwa mwaka kufikia mwaka wa 2030. Ripoti hiyo inabainisha kuwa kila dola 1 ya Marekani inayowekezwa kwenye uboreshaji huzalishia uchumi faida ya hadi dola 30 za Marekani.

Mifumo ya ekolojia inayohitaji kuboreshwa kwa dharura ni pamoja na mashamba ya kilimo, misitu, mbuga na savana, milima, maeneo ya mboji, maeneo ya mijini, maji safi, na bahari. Jamii zinazoishi katika takribani hekta bilioni mbili za ardhi iliyoharibiwa zinajumuisha watu masikini zaidi na waliotengwa.

"Ripoti hii inaonyesha kwa nini ni lazima sisi sote tuchukulie kwa uzito juhudi za uboreshaji ulimwenguni. Kwa kutumia ushahidi wa hivi karibuni wa kisayansi, inaelezea jukumu muhimu linalotekelezwa na mifumo ya ekolojia, kuanzia kwa misitu na mashamba hadi kwa mito na bahari, na inaonyesha hasara inayosababishwa na usimamizi mbaya wa sayari," Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Inger Andersen, na Mkurugenzi Mkuu wa FAO, QU Dongyu, waliandika kwenye dibaji ya ripoti hiyo.

"Uharibifu tayari umeathiri maisha ya watu wanaokadiriwa kuwa bilioni 3.2 - hiyo ni asilimia 40 ya jumla ya idadi ya watu ulimwenguni. Kila mwaka tunapoteza huduma za mifumo ya ekolojia zenye thamani ya zaidi ya asilimia 10 ya pato letu la uchumi kote duniani, "waliongeza, wakisisitiza kwamba" faida kubwa zinatungojea" kwa kubadili mwenendo huu. 

Uboreshaji wa mifumo ya ekolojia ni mchakato wa kukomesha na kukabiliana na uharibifu, utakaowezesha kuwa na hewa safi na maji safi, kupunguza hali mbaya mno ya hewa, kuboresha afya ya binadamu, na kuimarisha bayoanuai, pamoja na kuboreshi uchavushaji wa mimea. Uboreshaji unajumuisha shughuli mbalimbali, kuanzia kwa upandaji wa miti hadi kwa kurejesha maji kwenye maeneo ya mboji na matumbawe. Inachangia kutekelezwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu  (SDGs), ikijumuisha afya, maji safi, na amani na usalama, na malengo ya Mikataba mitatu ya 'Rio' kuhusiana na Hali ya Hewa, Bayoanuai na Majangwa.

Vitendo vinavyozuia, kusitisha na kukabiliana na uharibifu ni muhimu kufikia lengo la Mkataba wa Paris la kuzuia ongezelo la joto ulimwenguni lisizidi nyuzijoto 2. Uboreshaji, ukijumuishwa na kukomesha ubadilishaji zaidi wa matumizi ya mifumo asilia ya ekolojia, unaweza kusaidia kuzuia asilimia 60 inayotarajiwa ya uangamiaji wa bayoanuai. Unaweza kufanikiwa pakubwa kuwa na manufaa mengi kwa uchumi, jamii na ekolojia kwa wakati mmoja – kwa mfano, kilimo cha misitu pekee kina uwezo wa kuimarisha utoshelezaji wa chakula kwa watu bilioni 1.3, huku uwekezaji katika kilimo, utunzaji wa mikoko na usimamizi wa maji ukisaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na manufaa yakiwa mara nne zaidi ya uwekezaji uliofanywa.

Ufuatiliaji wa kuaminika wa juhudi za uboreshaji ni muhimu, kufuatilia maendeleo na kuvutia uwekezaji wa kibinafsi na wa umma. Ili kuunga mkono juhudi hizi, FAO na UNEP pia wanazindua leo Kituo cha Kidijitali cha Muongo wa Umoja wa mataifa, kinachojumuisha Utaratibu wa ufuatiliaji wa uboreshaji wa Mifumo ya Ekolojia. Utaratibu huo unawezesha nchi na jamii kupima maendeleo ya miradi ya uboreshaji kwenye mifumo muhimu ya ekolojia, ukisaidia kujenga umiliki na uaminifu katika juhudi za uboreshaji. Pia unajumuisha Jukwaa la Miradi ya Uboreshaji wa Maeneo Kame, ambalo linakusanya na kuchambua data, linashiriki mafunzo yaliyopatikana na kusaidia kubuni miradi ya kuboresha maeneo kame, na zana za angani za kutathmini maeneo bora ya kurejesha misitu.

Uboreshaji ni sharti uhusishe wadau wote wakiwemo watu binafsi, mashirika ya biashara, vyama, na serikali. La muhimu, lazima uheshimu mahitaji na haki za Watu wa Kiasili na jamii za wenyeji, na ijumuishe maarifa, uzoefu na uwezo wao ili kuhakikisha mipango ya uboreshaji inatekelezwa na kudumishwa.

MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia

Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia 2021-2030 unatoa wito wa kutunzwa na kuboreshwa kwa mifumo ya ekolojia kote ulimwenguni, kwa manufaa ya watu na mazingira. Unalenga kukomesha uharibifu wa mifumo ya ekolojia, na kuiboresha ili kufikia malengo yakimataifa. Baraza la Umoja wa Mataifa limetangaza Muongo wa Umoja wa Mataifa na unaongozwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa. Muongo wa Umoja wa Mataifa unaunda vuguvugu dhabiti lenye msingi mpana wa kimataifa ili kuimarisha uboreshaji na kuiwezesha dunia kuwa na hatima endelevu. Hiyo itajumuisha kuimarisha uwezo wa kisiasa wa uborejeshaji na maelfu ya miradi inayoendelea.

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa

UNEP in mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira ulimwenguni. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.

Kuhusu FAO

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ni shirika maalum la Umoja wa Mataifa ambao linaloongoza juhudi za kimataifa za kutokomeza njaa. Lengo letu ni kuwa na utoshelezaji wa chakula kwa watu wote na kuhakikisha kuwa watu wanapata chakula cha hali ya juu cha kutosha mara kwa mara ili kuwa na maisha mzuri, na watu wenye afya. Na nchi wanachama 197, FAO hufanya kazi katika nchi zaidi ya 130 ulimwenguni kote. Tunaamini kwamba kila mtu ana wajibu wa kutekeza kukomesha baa la njaa.

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Keisha Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, UNEP, +254 722 677747
Peter Mayer, Ofisa wa uhusiano mwema wa media wa FAO, +39 06 570 53304,