Elizabeth Maruma Mrema

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Naibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa


Wasifu

Tarehe 27 Desemba mwaka wa 2022, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alitangaza uteuzi wa Bibi Elizabeth Maruma Mrema wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Katibu Mkuu Msaidizi na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP). Alianza kufanya kazi yake tarehe 15 Februari mwaka wa 2023.

Kabla ya nafasi hiyo, Bi. Mrema alihudumu kama Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Mkataba wa Uanuai wa Kibayolojia kuanzia Juni mwaka wa 2020, akiwa amewahi kuhudumu kama kaimu katika nafasi hiyo tangu Desemba mwaka 2019. Kabla ya hapo, Bi. Mrema alihudumu katika nyadhifa mbalimbali katika miongo yake miwili ya kufanyia UNEP kazi, ikiwa ni pamoja na kama Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria na Naibu Mkurugenzi wa Kitengo cha Mifumo ya Ekolojia.

Kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka wa 2012, alihudumu kama Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Mkataba wa Uhifadhi wa Spishi za Wanyamapori wa Kuhamahama na pia aliwahi kuwa Kaimu Katibu Mtendaji wa UNEP/ASCOBANS (Mkataba wa Uhifadhi wa Mamalia Wadogo wa Majini katika Maeneo ya Baltic, Ireland na Bahari za Kaskazini) na pia kama Katibu Mtendaji wa Mkataba wa UNEP/Sokwe, yote akiwa mjini Bonn, Ujerumani.

Kabla ya kujiunga na UNEP, alifanya kazi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuacha akiwa Mshauri/Wakili Mwandamizi.  Akifanya kazi kwenye wizara, pia alikuwa mhadhiri wa Sheria ya Kimataifa ya Umma na Diplomasia ya Mikutano katika Kituo cha Mahusiano ya Nje na Diplomasia cha Tanzania. Pia aliwahi kuwa mhadhiri mgeni asiyelipwa katika Kitengo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Nairobi na hapo awali katika Shirika la Kukuza Sheria za Kimataifa (IDLO), mjini Rome, Italia.

Wakili na mwanadiplomasia kitaaluma na LLB (Shahada) kutoka Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, Tanzania, LLM kutoka Chuo Kikuu cha Dalhousie, Kanada na Stashahada baada ya Shahada ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia (Summa Cum Laude) kutoka Kituo cha Mahusiano ya Kigeni na Diplomasia mjini Dar-es-Salaam, Tanzania.  Katika mwaka wa 2021, Tume ya Dunia ya Sheria ya Mazingira ya IUCN (WCEL), kwa ushirikiano na UNEP, ilimtunuku Bi Mrema Tuzo la Nicholas Robinson kwa Ufanisi wa Sheria ya Mazingira.  Tuzo hili la kifahari lilitolewa kwa kutambua mafanikio yake kikazi, ya kuendeleza sheria za mazingira.  Katika mwaka wa 2022, pia alitunukiwa thTuzo la Kimataifa la Kew kwa kazi yake ya kutunza mazingira na ameorodheshwa kwenye Wanawake wa Kiafrika Wenye Ushawishi Zaidi Mwaka wa 2021 na 2022 kama alivyochaguliwa na Avance Media.

Yeye pia ni mwenyekiti mwenza wa Kikosi Kazi cha Ufichuzi wa Kifedha unaohusiana na Mazingira.

UNEP Deputy Executive Director Elizabeth Maruma Mrema

Ungana na Elizabeth Maruma Mrema


The Latest

Hotuba
Kukuza ushirikiano ili kukabiliana na changamoto za mazingira barani Afrika

Kwa takribani miaka 40, Kongamano la Mawaziri wa Afrika kuhusu Mazingira limetumika kama kurunzi ya kuelekeza wakati wa nyakati hatari kwa mazingira. Limesaidia bara lenye uanuai kufikia maafikiano kuhusu vitisho vikuu zaidi kwa sayari yetu - na kuwezesha Afrika kusikika zaidi katika jukwaa la kimataifa. More