Kazi yetu Afrika

Afrika imetunikiwa na maliasili nyingi inayojumuisha ardhi ya kilimo, maji, mafuta, gesi asili, madini, misitu na wanyama pori. Bara hili lina kiwango kikubwa cha maliasili duniani, ikiwa ni pamoja na nishati jadidifu na nishati isiyokuwa jadidifu.

Afrika ni makazi ya: asilimia 30 ya hazina ya madini duniani, asilimia 8 ya gesi asili duniani, asilimia 12 ya hifadhi za mafuta duniani. Bara hili lina asilimia 40 ya madini duniani na asilimia 90 ya kromiamu na platinamu. Hifadhi kubwa zaidi ya kobalti, almasi, platinamu na urani duniani, hupatikana Afrika. Katika ngazi ya dunia, Afrika ina asilimia 65 ya aridhi ya kilimo na asilimia 10 ya maji safi yanayoweza kuzalisha nishati jadidifu.

Katika nchi nyingi za Afrika, hazina ya maliasili ni kati ya asilimia 30 na 50 ya jumla ya mali yake. Zaidi ya asilimia 70 ya watu wanaoishi kusini mwa Jangwa la Sahara wanategemea misitu na mapori kupata riziki zao. Ardhi ina manufaa ya kukuza uchumi na pia ni rasilimali ya kuendeleza utamaduni wa jamii. Hata hivyo, asili mia kubwa ya rasilimali hii hutumika kwa njia isiyodumisha uendelevu na baadhi hupotea kupitia kwa shughuli zilizo kinyume cha sheria. Hii inamaanisha ya kwamba manufaa yanayotokana na rasilimali hizi yanaendelea kupungua miaka inapoendelea kusonga mbele. Kwa mfano, kila mwaka, Afrika hupoteza takribani dola bilioni 195 ya mali yake asili kupitia kwa biashara haramu, uchimbaji wa migodi kinyume cha sheria, ukataji wa miti kinyume cha sheria, biashara haramu ya wanyama pori, uvuvi usiodhibitiwa, uharibifu wa mazingira, udidimiaji wake na kadhalika.

Kwa jumla, bara linapata manufaa mengi kwa kushirikiana na kuweka pamoja maliasili yake ili kufadhili ajenda yake ya maendeleo ya kuongeza utajiri wake. Pia, ni sharti lihakikishe kuwa ukuzaji na matumizi ya maliasili yake unaleta manufaa, hauthiri hali ya hewa na ni wa njia endelevu.

Kongamano Kuhusiana na Mazingira la Mawaziri Kutoka Afrika (AMCEN) linatambua ya kuwa maliasili ni nguzo kwa uchumi wa bara na kudhibitisha kuwa iwapo maliasili itatumiwa kuzalisha mali na kama mbinu ya uwekezaji, itasaidia kufikia Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya 2030 kuhusiana na Maendeleo Endelevu na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), na Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063 kupitia mchango wa kifedha, kiuchumi, kijamii na wa kimazingira.

Kazi ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa

 GEO-6 Tathmini ya Eneo la Afrika inadokeza kuwa mazingira yanadidimia kwa kasi kuliko ilivyodhaniwa hapo awali. Inasitiza ya kwamba serikali zinapaswa kufanya uamuzi kwa kasi ili kusitisha hali hii. Ripoti inatambua kuwa kuna maliasili Afrika na inadokeza kuwa ukuwaji wa uchumi barani Afrika unategemea kuhifadhi maliasili yake kwa njia endelevu. Hata hivyo, matumizi ya maliasili ya Afrika kwa njia zisizo endelevu na idadi ya watu wanaongezeka kila uchao, na uzembe wa watu walio na mamlaka ya kuunda sera mwafaka na sheria za kukabiliana na matumizi mabaya ya rasilimali hizi na hata kuzitumia zaidi ya uwezo wake inazua changamoto. Ulimwengu unaonyesha kuna hatari, kama inavyodhibitishwa na kuwepo kwa majanga mengi yasiyodhibitiwa. Hali hii inachangia kukosekana kwa chakula cha kutosha, ukosefu wa maji, kuwepo kwa magonjwa, mizozo, uhamaji na umaskini. Mambo haya yote yanaweza kuyumbisha chumi.

Kufikia maendeleo endelevu barani Afrika

Ili Afrika iweze kupata manufaa ya kiuchumi na ya kijamii kutokana na maliasili hii, ni muhimu kushughulikia kwa dharura masuala kama vile utunzaji wa rasilimali, athari zake kwa uchumi na kwa mazingira iwapo zitatumika kwa njia endelevu.

Afisi ya eneo la Afrika husaidia serikali za Afrika kutekeleza maamuzi na maafikiano kuhusiana na maliasili. Pia, husaidia kupata masuluhisho ya uvumbuzi katika viwango vya kimaeneo, kitaifa na maeneo ya mashambani kwa manufaa ya umma. Kwa hivyo, itazalisha mali na kubuni nafasi za kazi, itasaidia katika ukusanyaji wa kodi, kusababisha usalama wa chakula, kusababisha usawa katika jamii na kuwa na mazingira mazuri.