20 Jul 2020 Toleo la habari

Watu thelathini na tano wachaguliwa kuwakilisha kanda zao kwenye fainali ya kuwania tuzo la Vijana Bingwa Duniani

  • Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa leo lilitangaza majina ya watu thelathini na tano wanaowakilisha kanda zao kuwania tuzo la Vijana Bingwa Duniani. Ni tuzo la kiwango cha juu zaidi linalotolewa kwa vijana na Umoja wa Mataifa.   
  • Kikosi cha waamuzi wa kimataifa kitachagua wasindi saba kila mmoja kutoka kila kanda huku kanda ya Asia ya Pasifiki ikiwakilishwa na watu wawili. Washindi watatangazwa Disemba.
  • Washindi hupokea ufadhili wa dola za Marekani 10,000 na msaada wanaohitaji ili kufanikisha mawazo yao.

Nairobi, Julai 20, 2020 – Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) leo lilitangaza majina ya watu thelathini na tano wanaowakilisha kanda zao kwenye fainali ya kuwania tuzo la Vijana Bingwa Duniani.  Shindano hilo la kimataifa linalenga kutafuta, kusaidia na kusherehekea watu binafsi wa kipekee wenye umri kati ya miaka 18 na 30 walio na maono makubwa ya kutunza au kuboresha mazingira.  

Wanafainali 35 wa kiwango cha juu - waliochaguliwa kutoka kwa watu 845 waliotuma maombi ya kushiriki ili kuwakilisha kanda zao - walichaguliwa kutokana na mtindo wao mpya wa kushughulikia changamoto zinazokumba mazingira kupitia njia za kisasa, za kiubunifu na zilizo na manufaa mengi.

Kuanzia kwa utunzaji wa ardhi ya kiasili ya Amazon kupitia usafiri wa kujiburudisha, hadi kwa kubadilisha gesi chafu na kuifanya bidhaa muhimu kule Marekani, hadi kwa ukusanyaji wa plastiki Ugiriki na uzalishaji wa kawi kutoka kwa maji nchini Nijeria, wanafainali wanashughulikia changamoto mbalimbali za mazingira na wana uwezo wa kuleta mabadiliko.

"Licha ya changamoto kutokana na janga la COVID-19, masuluhisho makuu yaliyotolewa na wawaniaji katika fainali ya mwaka huu ni ya kipekee. Ni wazi kuwa janga hili halikusitisha uhamasishaji wa kuboresha dunia.  Badala yake, limetukumbusha ni kipi kilicho hatarini tunapong'ang'ana kuboresha sayari yetu. Pia, inaonyesha umuhimu wa kujiimarisha baada ya korona kutatusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kutunza binadamu na kuhifadhi mazingira," alisema Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Inger Andersen.

"Vijana kote ulimwenguni wanahamasisha kuhusu maamuzi mabaya tuliyofanya na athari ya uharibifu wa mazingira kwa mustakabali wao," aliongezea.  "Tumejitolea kusaidia vijana kusikika, kuwapa jukwaa na fursa ya kufanikisha juhudi zao huku tukiendelea kutia motisha mamilioni ya vijana kote ulimwenguni." 

Washindi saba wanaowakilisha kanda zao watachaguliwa na waamuzi wa kimataifa wanaoshirikisha Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Inger Andersen; Mjumbe wa Vijana wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jayathma Wickramanayake; Muungaji Mkono wa Chumi Bunifu wa UNEP, Roberta Annan, na Afisa Mkuu Mtendaji wa Wakfu wa Umoja wa Mataifa, Elizabeth Cousens. 

Kila mshindi hupokea ufadhili wa dola za Marekani 10,000, msaada wanaohitaji na pia huweza kupata majukwaa makuu na washauri.  Tuzo la Vijana Bingwa Duniani hufadhiliwa na Covestro.

Mhutasari kuhusu wanafainali 35 wanaowakilisha kanda zao na muhtasari kuhusu mawazo yao, ikijumuisha video zao vinapatikana kwenye wavuti ya Vijana Bingwa Duniani. Waamuzi wa kimataifa watachagua washindi wa tuzo la Vijana Bingwa mwezi wa Disemba na watasherehekewa wakati wa sherehe ya UNEP inayoadhimishwa kila mwaka inayojumuisha Mabingwa wa Dunia.

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Vijana Bingwa Duniani
Vijana Bingwa Duniani ni tuzo linasherehekea vijana walio na mawazo makuu ya kutunza na kuboresha mazingira, walio na maono ya kuwa na mustakabali endelevu na walio na mazoea ya kuleta mabadiliko.  Wana kila kitu kinachohitajika kuwafanya Vijana Bingwa Duniani.  Hawaogopi kutofaulu na wanaamini kuwa kuna uwezekano wa kuwa na sayari nzuri katika siku zijazo.

Kuhusu Covestro

Covestro ni kinara kwenye biashara ya vifaa vya polima duniani.  Kampuni hiyo huunda vifaa vya kiwango cha juu kutoka kwa polima na ketengeneza bidhaa kwa njia bunifu, vifaa ambavyo tunatumia katika shughuli nyingi za maisha yetu ya kila siku. Vifaa hivyo hutumika katika sekta ya usafiri, katika sekta ya ujenzi, katika utengenezaji wa mbao na fanicha, na katika viwanda vya vifaa vya kiekitroniki.   Sekta nyinginezo ni kama vile spoti na burudani, sekta ya vipodoshi, sekta ya afya na ya kemikali.  Covestro ina viwanda 30 kote duniani na imeajiri watu zaidi ya elfu 16,000.

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa
UNEP in mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Georgina Avlonitis, Vijana Bingwa Duniani, UNEP

Keishamaza Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, UNEP