15 Jun 2019 Toleo la habari Malengo ya Maendeleo Endelevu

Raia wa Denmark Inger Andersen achukua usukani kama mkuu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa

Nairobi, 15 Juni 2019 –Mtaalamu wa masuala ya uchumi na mazingira Inger Andersen ameanza kazi yake mpya leo kama Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, huku akiahidi kutoa kiapaumbele kwa ukabilianaji wa mabadiliko ya tabia nchi.

Bi. Andersen aliteuliwa kuchukua wadhifa huo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na kuidhinishwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mnamo Februari mwaka wa 2019.

"Nina furaha na ninajivunia kuanza kazi katika Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa katika nchi inayovutia ya Kenya na katika kipindi muhimu sana ulimwenguni," alisema Bi. Andersen. "Hakuna wakati ambapo usimamizi mzuri wa mazingira umekuwa na umuhimu kuliko sasa. Mabadiliko ya tabia nchi, kuangamia kwa bayoanwai na uchafuzi kwa viwango vyake vyote, kwa sasa inahatarisha wazi afya ya binadamu na sayari, na kuathiri pia utajiri.

"Nisingekubali kazi hii iwapo ningekosa matumaini. Kutokana na uchunguzi wa kimazingira na wa kisayansi tunafahamu kuwa inawezekana kabisa kwa binadamu kutatua matatizo tuliyosabisha. Sasa, kushinda wakati mwingine wowote, kuna haja ya kuyashughulikia. Haya yanadhihirika wazi kutokana na ongezeko la kujitolea kwa serikali, kuimarika kwa ushirikiano kutoka sekta za kibinafsi, na pia kuchipuka kwa makundi kote duniani yasiyoweza kudhibitiwa yanayoongozwa na vijana wanaotaka mabadiliko.

"Kwa majuma yajayo na miezi ijayo, nitafanya kazi na wafanyikazi bora walijitolea wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, pamoja na wabia na wafadhili wetu ili kuweka wazi mambo yanayopewa kipaumbele na shirika ambalo ni muhimu kwa matamanio yetu ya kuwa na dunia endelevu na yenye usawa.

"Ninachoweza kusema sasa ni kuwa, kifaa muhimu tulicho nacho sasa ni umoja ulimwenguni. Na kwa changamoto kubwa kama zile tunazozipitia wote, tutafaulu pamoja au tutashindwa pamoja. Ninatarajia kuimarisha ushirikiano na wabia wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, wageni na wa zamani, kufanya kazi ili kuweko na mazingira yanayowezesha viumbe vyote kunawiri.

Bi. Andersen anaingia afisini akiwa mpenzi wa kuhifadhi mazingira na wa maendeleo endelevu. Hali hii inadhihirika kutokana na kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 30 kwenye maendeleo ya kimataifa ya uchumi, utunzaji wa mazingira na uundaji wa sera, kuanzisha na kuendeleza miradi inayozalisha matokeo.

Kati ya Januari 2015 na Mei 2019, Bi. Andersen alikuwa mkurugenzi mwendeshaji wa Muungano wa Kimataifa wa Kuhifadhi Mali Asili (IUCN). Kabla ya kujiunga na (IUCN), Bi. Andersen alishikilia nyadhifa mbalimbali katika Benki ya Dunia: alihudumu kama Naibu wa Rais wa Mashariki ya Kati na Kusini mwa Afrika, Naibu wa Rais wa Maendeleo Endelevu, na kama Mkuu wa Mfuko wa Kamisheni ya Vituo Vya  Kimataifa vya Utafiti wa Kilimo (CGIAR).

Kabla ya kujiunga na Benki ya Dunia, Bi. Andersen alifanya kazi na Umoja wa Mataifa kwa miaka 12. Alianzia katika afisi ya Umoja wa Mataifa ya Sudano-Sahelian, akiwajibikia ukame na masuala yanayohusiana na majangwa kabla ya kuteuliwa kama Mratibu wa Maji na Mazingira wa Mpango wa Mandeleo wa Umoja wa Mataifa katika Eneo la Uarabu .

Historia ya Elimu ya Bi. Andersen ya kimasomo ni pamoja na Shahada ya kwanza ya BA kutoka chuo kikuu cha London Metropolitan University North na shahada ya Uzamili ya MA kutoka School of Oriental and African Studies kutoka Chuo kikuu cha London, hasa akisomea maendeleo ya uchumi.

Anachukua usukani kutoka kwa Joyce Msuya, kutoma Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, ambaye amefanya kazi kama kaimu mkuu wa shirika hili tangu mwishoni mwa mwaka jana. Bi. Msuya ataendelea kama Naibu wa Mkurugenzi Mtendaji.

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa- lenye makao yake makuu Nairobi, Kenya- hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika kutunza mazingira kupitia kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.

 

Kwa maelezo zaidi na kupanga mahojiano, tafadhali wasiliana na:

Keishamaza Rukikaire Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, UNEP