Photo: UNEP
19 Apr 2024 Tukio Kushughulikia Mazingira

Njia tano unazoweza kutumia kusaidia kuokoa mazingira Siku hii ya Mama Dunia

Ni rahisi kukatishwa tamaa na hali ya sayari.   

Binadamu anavunja rekodi zote mbaya kuhusu ongezeko la joto duniani. Mifumo dhaifu ya ekolojia inakabiliwa na shinikizo kubwa. Zaidi ya mimea wanyama na viumbe hai wengine milioni 1, wako hatarini kuangamia. Hewa chafu na uchafuzi wa kemikali vinatishia ardhi, bahari na afya yetu. 

Lakini Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia, tarehe 22 April, ni ukumbusho kwamba kuna mengi tunayoweza kufanya, kama watu binafsi, ili kukabiliana na majanga ya aina tatu duniani ya mabadiliko ya tabianchiuharibifu wa mazingira na bayoanuai, na uchafuzi na taka

"Kila hatua, hata iwe kubwa au ndogo, ni muhimu kwa sayari," alisema Bruno Pozzi, Naibu Mkurugenzi wa Kitengo cha Mifumo ya Ekolojia cha Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).  "Dharura ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na uchafuzi mbaya zaidi wa mazingira ni visivyoweza kupuuzwa. Tunaweza kubadili hali ya kudorora kwa Dunia lakini tunahitaji kuja pamoja na kila mmoja wetu kutekeleza wajibu wake."   

UNEP imetengeneza zana za nyenzo za kuchukua hatua za kushughulikia mazingira kuhusiana na masuala mbalimbali. Hapa kuna mwongozo kuhusu masuala tano kati yake: 

1. Uisha mifumo ya ekolojia inayokidhi mahitaji yetu  

A woman holds a small machete in a field in Madagascar
Picha: UNEP

Je, wajua kuwa duniani zaidi ya hekta bilioni 2 za ardhi zimeharibiwa? Au kuwa idadi na muda wa ukame kudumu umeongezeka kwa asilimia 29 tangu mwaka wa 2000. Kupata masuluhisho kwa matatizo haya ulimwenguni ni muhimu.  Siku ya Mazingira Duniani tarehe 5 Juni itaangazia uboreshaji wa ardhi, kuenea kwa majangwa na kustahimili ukame. Mwongozo wa Uboreshaji wa Mifumo ya Ekolojia: Mwongozo wa Vitendo vya Kuponya Sayari unaelezea mbinu za kurejesha aina nane muhimu ya mifumo ikolojia - misitu, mashamba, maeneo yaliofunikwa na nyasi na maenao ya savana, mito na maziwa, bahari na maeneo ya pwani, miji na majiji, maeneo ya mboji na milima. Kwa kuchukua hatua hizi zinazopendekezwa, unaweza kuwa sehemu ya #GenerationRestoration!  

2. Hamasisha kuhusu mabadiliko ya tabianchi 

Fishermen at work on Kenya’s lake Turkana   
Picha: UNEP/Duncan Moore

Ulimwengu unakabiliwa na dharura ya tabianchi, "ishara ya hatari kwa wanadamu," kwa mjibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Uzalishaji wa gesi ya ukaa usipopungua mno, ongezeko la joto linaweza kupita nyuzijoto 2.9 katika karne hii. Kampeni ya UNEP ya Chukua Hatua Sasa: Hamasisha inaonyesha jinsi wananchi wanavyoweza kulazimisha serikali na mashirika ya biashara kufikia aina ya mabadiliko ya kimfumo yanayohitajika ili kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzijoto 1.5 zaidi ya viwango vya kabla ya kuanza kwa viwanda.  

3. Komesha mlima wa plastiki duniani  

A man cleans plastic from a beach in the Republic of Côte d’Ivoire
Picha: UNEP/Ollivier Girard 

Plastiki imetapakaa kila mahali. Iko katika mavazi yetu, vifaa vya kutumia nyumbani, vifaa vya watoto kuchezea, vifaa vya kufungia chakula, vifaa vya matibabu...orodha hii inaendelea. Ingawa plastiki ina matumizi mengi, mazoea yetu ya kutumia plastiki inayotumika mara moja hudhuru sayari. Inaweza kuchukua maelfu, au maelfu na maelfu, ya miaka kuoza. Hata hivyo tunaendelea kuzalisha na kutumia tani milioni 430 za plastiki kwa mwaka, theluthi mbili kati yake hujikuta haraka kwa taka zinazotupwa kwenye madampo na kuchafua maziwa, mito, udongo na bahari.    

Kwa kufahamu athari za plastiki kwa mabadiliko ya tabianchi, mifumo ya ekolojia, wanyamapori na uchumi, Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa zilikubaliana kuhusu azimio la kuunda a chombo cha kisheria kufikia mwaka wa 2024 cha kukomesha uchafuzi wa plastiki. Tunapoelekea mkutano wa nne wa Kamati ya Majadiliano ya Serikali Mbalimbali (INC) kuhusu makubaliano ya kimataifa Mpango wa UNEP: Ni wakati wa kukomesha uchafuzi wa plastiki zana za uchafuzi wa plastiki zinaelezea kile ambacho watu binafsi wanaweza kufanya ili kusaidia kukomesha janga hili kwa mazingira. Hii ni pamoja na kupunguza plastiki isiyohitajika, kuchagua kutumia tena badala ya kununua bidhaa mpya, kuunga mkono kampuni zinazounda upya plastiki na kujaribu kupunguza matumizi ya plastiki inayotumika mara moja, na kuziomba serikali kupitisha sera za uchumi unaotumia bidhaa tena na tena na kuimarisha mifumo ya kushughulikia taka. 

4. Kupiga marufuku hewa chafu kutoka angani   

A 70-year-old car is parked on a dirt road in Harar, Ethiopia
Picha: UNEP/Duncan Moore

Zaidi ya asilimia 99 ya watu duniani huvuta hewa isiyo salama. Uchafuzi wa hewa ndio hatari kubwa zaidi kwa afya nyakati zetu, na husababisha vifo vya mapema vya takribani watu milioni 7 kila mwaka. Kukumbana na hewa chafu pia kunaweza sababisha magonjwa ya moyo na mapafu, saratani ya mapafu na kiharusi na magonjwa mengine. Vichafuzi vya hewa pia hudhuru mazingira yetu asilia, hupunguza usambazaji wa oksijeni katika bahari zetu, na kuifanya kuwa vigumu kwa mimea kukua na kuchangia janga la mabadiliko ya tabianchi.  Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na anga za bluu tarehe 7 Septemba inalenga kuhamasisha kuhusu tatizo hili, huku mwongozo unaoingiliana wa UNEP ukifafanua hatua unazoweza kuchukua ili kupelekea kuwa na hewa safi. 

5. Panda miti mwafaka, usikosee 

Mangrove seedlings are seen at a nursery in Kenya
Picha: UNEP/Stephanie Foote

Miti ni ya ajabu." Hufyonza hewa ya ukaa kutoka angani, hulinda na kurutubisha udongo, ni chanzo cha kuni na mbao, na hutoa makazi kwa wanyama, ndege na wadudu wengi. Si ajabu kuwa upandaji miti, kuboresha mifumo ya ekolojia na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, vimekuwa maarufu sana. Lakini sio rahisi kama inavyosikika. Kwa mfano, kupanda miti isiokuwa mwafaka mahali pasipofaa kunaweza kudhuru bayoanuai na kusababisha kila aina ya matokeo yasiyokusudiwa. Upandaji Miti na uboreshaji wa mfumo ya ekolojia: kozi ya kina ya UNEP inaweka kanuni tano za msingi za kufanya usikosee.  

 

Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia iinaadhimishwa kote ulimwenguni tarehe 22 April. Haya ni madhimisho ya tatu ya Siku ya Mama Dunia inayoadhimishwa chini ya Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia.   

Kuhusu Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia   

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limetangaza mwaka wa 2021 hadi wa 2030 kama Muongo wa UN wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia. Muongo unaoongozwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa na Shirika la Chakula na Kilimo, kwa ushirikiano wa wabia, unalenga kuzuia, kusitisha, na kukukabiliana na uharibifu na kudidimia kwa mifumo ya ekolojia kote duniani. Unalenga kuboresha mabilioni ya hekta ya ardhi ya nchi kavu pamoja na mifumo ya ekolojia ya majini. Wito wa kimataifa wa kuchukua hatua, Muongo wa Umoja wa Mataifa unaungwa mkono na wanasiasa, utafiti wa kisayansi, na ufadhili ili kuimarisha uboreshaji.