Lance Asper/Unsplash
30 Aug 2021 Toleo la habari Usafiri

Kipindi cha kutumia petroli iliyo na risasi kimekwisha, hali inayoondoa hatari kuu kwa ubora wa sayari na afya ya binadamu

  • Kukomeshwa rasmi kwa matumizi ya petroli iliyo na risasi kutazuia vifo vya mapema takribani milioni 1.2 na kuokoa dola za Marekani milioni 2.44 kwa mwaka
  • Kukomeshwa kwa matumizi ya petroli iliyo na risasi kunatokana na kampeni ya miaka 19 ilyoendeshwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na wabia wenza.
  • UNEP inatoa wito kwa nchi kufanya kazi kuhakikisha zinatumia magari yasiozalisha hewa chafu ili kushughulikia zaidi uchafuzi wa hewa na mabadiliko ya tabianchi

 

Nairobi, Agosti 30, 2021 – Wakati vituo vya huduma nchini Algeria vilipoacha kuzalisha petroli iliyo na risasi mwezi wa Julai, matumizi ya petroli iliyo na risasi yalimalizika ulimwenguni kote. Hii inatokana na kampenin iliyoendeshwa karibu miongo miwili na Ubia wa kimataifa uliongozwa na UNEP wa Nishati na Magari Yasiyochafua Mazingira (PCFV).

Tangu mwaka wa 1922, kuongeza 'tetraethyllead' kwa petroli ili kuboresha utenda kazi wa injini kumekuwa janga kwa mazingira na afya ya umma. Kufikia miaka ya 1970, karibu petroli yote iliyozalishwa ulimwenguni kote ilikuwa na risasi. Wakati Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) lilipoanza kampeni yake ya kuondoa risasi kwenye petroli katika mwaka wa 2002, ilikuwa mojawapo ya vitisho hatari mno vya mazingira kwa afya ya binadamu.

Mwaka wa 2021 umeashiria mwisho wa petroli iliyo na risasi ulimwenguni, baada ya kuchafua hewa, vumbi, udongo, maji ya kunywa na mazao ya chakula kwa sehemu kubwa ya karne. Petroli iliyo na risasi husababisha ugonjwa ya moyo, kiharusi na saratani. Pia inaathiri ukuaji wa ubongo wa mwanadamu, hasa kudhuru watoto, huku tafiti zikidokeza hupunguza IQ na alama kati ya 5 na 10. Kupiga marufuku matumizi ya petroli iliyo na risasi kumekadiriwa kutazuia vifo vya mapema zaidi ya milioni 1.2 kwa mwaka, kuongeza alama za IQ kwa watoto, kuokoa dola za marekani trilioni 2.44 kwa uchumi ulimwenguni, na kupunguza viwango vya uhalifu.

"Utekelezaji mzuri wa marufuku ya petroli iliyo na risasi ni hatua kubwa kwa afya duniani na kwa mazingira yetu," Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP. “Kukabiliana na karne ya vifo na magonjwa yaliyoathiri mamia ya mamilioni ya watu na kuharibu mazingira ulimwenguni kote, tunahamasishwa kubadili mwelekeo wa wanadamu kuwa bora kwa kuimarisha mabadiliko kuelekea magari yasiyochafua mazingira na yanayotumia umeme.”

Kufikia miaka ya 1980, nchi nyingi zenye kipato cha juu zilikuwa zimepiga marufuku matumizi ya petroli iliyo na risasi, lakini hadi kufikia mwaka wa 2002, karibu nchi zote za kipato cha chini na cha kati, ikijumuisha baadhi ya wanachama wa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD), bado walikuwa wanatumia petroli iliyo na risasi. PCFV ni ubia wa umma na wa sekta binafsi uliowaleta wadau wote pamoja, ikitoa msaada wa kiufundi, kuhamasisha, kukabiliana na changamoto za kieneo na upinzani kutoka kwa wafanyabiashara wa mafuta na wazalishaji wa risasi, na pia kuwekeza katika uboreshaji wa kuyasafisha.

Dkt Kwaku Afriyie, Waziri wa Sayansi ya Mazingira, Teknolojia na Ubunifu nchini Ghana, alisema "Wakati UN ilipoanza kufanya kazi na serikali na wafanyabiashara kukomesha matumizi ya risasi kwa petroli, mataifa ya Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara yalipokea kwa furaha fursa hii. Ghana ilikuwa mojawapo ya nchi tano za Afrika Magharibi kujiunga na warsha na matamko ya kimaeneo mapema. Kufuatia kampeni za vyombo vya habari vya PCFV, ripoti, tafiti, zilizofichua ukiukaji wa sheria, na upimaji wa maeneo ya umma uliofanywa uliofichua viwango vya juu vya risasi katika damu ya watu wengi, Ghana iliazimia zaidi kuondoa risasi kwa mafuta yake. "

Licha ya maendeleo haya, ongezeko la magari duniani linaendelea kuchangia hatari kwa hewa, maji na uchafuzi wa ardhi kwa eneo husika, na kwa changamoto ya hali ya hewa duniani: sekta ya uchukuzi huchangia takribani robo ya uzalishaji wa gesi chafu kutokana na nishati na inatarajiwa kuongezeka hadi theluthi moja kufikia mwaka wa 2050.

Ijapokuwa nchi nyingi zimeanza kutumia magari ya umeme, Magari mapya bilioni 1.2 yatakuwa barabarani katika miongo ijayo, na mengi kati ya haya yatatumia mafuta ya visukuku, haswa katika nchi zinazoendelea. Hii ni pamoja na mamilioni ya magari duni yaliyotumika yanayosafirishwa kutoka Ulaya, Marekani na Japani, hadi kwa nchi za kipato cha kati na cha chini. Hii inachangia ongezeko la joto duniani na mawimbi yanayochafua hewa na kuwa na uwezekano wa kusababisha ajali.

"Ukweli kwamba muungano unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa wa serikali, mashirika ya biashara na mashirika ya uraia uliweza kufanikiwa kuondolea ulimwengu mafuta haya yenye sumu ni ushahidi wa nguvu za ushirikiano wa kimataifa kuwezesha dunia kuwa na hatima endelevu na safi isiyochafua mazingira," Bi Andersen alisema. "Tunawahimiza wadau hawa kuchochewa na mafanikio haya makubwa ili kuhakikisha kuwa kwa sasa kwa vile kuna mafuta yasiyochafua mazingira duniani, tuanze kutumia viwango vya magari yasiyochafua mazingira ulimwenguni - mchanganyiko wa mafuta yasiyochafua mazingira na magari yasiyochafua mazingira vinaweza kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kwa zaidi ya asilimia."

Kwa kuongezea, ijapokuwa sasa tumeondoa chanzo kikuu zaidi cha uchafuzi wa risasi, hatua za dharura bado zinahitajika ili kukomesha uchafuzi wa risasi kutoka kwa vyanzo vinginevyo - kama vile kwenye rangi iliyo na risasi, betri zilizo na risasi, na risasi kwenye vitu vinavyotumiwa majumbani.

Kukomesha kwa matumizi ya petroli iliyo na risasi kunalenga kuwezesha kufikia mengi ya Malengo ya Maendeleo Endelevu, ikijumuisha afya na maisha mema (SDG3), maji safi (SDG6), nishati isiyochafua mazingira (SDG7), miji endelevu (SDG11), ushughulikiaji wa mazingira (SDG13) na maisha kwenye ardhi (SDG15). Pia inatoa fursa kwa uboreshaji wa mifumo ya ekolojia, haswa katika mazingira ya mijini, ambayo yameharibiwa na uchafuzi huu wa sumu. Mwishowe, inaashiria maendeleo makubwa tunapoelekea maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na angaa za bluu tarehe 7 Septemba.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Ubia wa Nishati na Magari Yasiyochafua Mazingira (PCFV):

Katika mwaka wa 2002, Ubia wa Nishati na Magari Yasiyochafua Mazingira (PCFV) ulianzishwa wakati wa Mkutano Mkuu wa Dunia wa Maendeleo Endelevu. UNEP ilikuwa mwenyeji wa Sekretarieti hiyo na lengo la kukomesha matumizi ya petroli iliyo na risasi duniani na ilitoa msaada kwa nchi nyingi na miradi ya kikanda. Wakati huo, nchi 117 ulimwenguni kote zilikuwa bado zinatumia petroli iliyo na risasi huku nchi 86 zikiunga mkono kukomesha matumizi ya petroli iliyo na risasi. Katika mwaka wa 2006, mafanikio makuu ya kwanza yalipatikana - Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara ilikomesha matumizi ya petroli iliyo na risasi. Nchi ya mwisho kufanya mabadiliko ilikuwa Algeria katika mwezi wa Julai mwaka wa 2021.

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP):

UNEP in mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira ulimwenguni. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.    

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Keisha Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa,