22 Sep 2020 Toleo la habari Kushughulikia kemikali na uchafuzi

Kupitisha ujumbe: Flipflopi kuendeshwa kwenye Ziwa Victoria katika safari ingine ya kipekee

  • Flipflopi, mashua kubwa mno duniani ya kwanza kutengenezwa kutoka kwa taka ya plastiki iliyokusanywa mijini na fukweni nchini kenya, inasafiri kuelekea Ziwa Victoria ili kuhamasisha kuhusu uchafuzi unaoathiri mfumo wa ekolojia wa maji safi katika eneo hilo.
  • Mbali na mradi huo ni wito unaotolewa kwa nchi zote Wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki kukubaliana kukomesha matumizi ya plastiki isiyohitajika inayotumika tu mara moja.
  • Mashua hiyo itawasili mjini Kisumu tarehe 22 mwezi wa Septemba na itahifadiwa na Shirika Linalohudumia Wanyamapori nchini Kenya (KWS) kwenye mbuga ya Impala. Umma utaruhusiwa kwenda kuitazama.

 

Nairobi, Septemba 22, 2020 - Takribani miezi 18 baada ya Flipflopi kufanya safari yake ya kwanza ya kihistoria kutoka Lamu, nchini Kenya, hadi Zanzibar, nchini Tanzania, mashua ya kwanza kutengenezwa duniani kwa asilimia 100 kutoka kwa taka ya plastiki iko tayari kwa safari ingine ya kihistoria, wakati huu kwenye Ziwa Victoria.

Safari ya Ziwa Victoria imewezeshwa na serikali za Kenya, Uganda na Tanzania, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), UN Live na sekta za binafsi kama vile Waterbus.

Kwa kipindi cha miezi minne mwanzoni mwa mwaka wa 2021, chombo hicho kitasafiri katika Ziwa Victoria, Ziwa kubwa mno lenye maji safi barini Afrika ili kuonyesha athari za uchafuzi wa mifumo muhimu ya ekolojia, na kushirikisha serikali, viongozi katika jamii, wanamazingira, na wanafunzi kutafuta suluhu mwafaka kwa kero linalotokana na uchafuzi.

"Lengo la safari yetu ijayo ni kufikisha ujumbe wetu mbali, kutoka kwetu pwani eneo la Lamu, hadi kwa ndugu zetu nchini Kenya, Tanzania, na Uganda, wanaoishi karibu na Ziwa Victoria. Tuna matumaini kuwa safari hii kwenye Ziwa Victoria itaweza kusaidia kufanya uamuzi uaohitajika zaidi wa kuchukua hatua dhidi ya uchafuzi mbaya mno unashuhuduwa kwenye mfumo wa ekolojia muhimu wa maji safi katika eneo hilo," alisema Ali Skanda, mwanzilishi mwenza wa mradi wa Flipflopi.

Tangazo kuhusu safari kwenye Ziwa Victoria lilitolewa leo wakati wa mkutano na vyombo vya habari ulioandaliwa na UNEP, AFD, UN Live, Wizara ya Mazingira na Misitu na ile ya Utalii na Wanyamapori nchini Kenya. 

"Safari ya Flipflopi kwenye Ziwa Victoria inapitisha ujumbe muhimu kwa njia inayoeleweka kwa urahisi kwa serikali, serikali za mitaa, wadau na jamii za eneo hilo - okoa Ziwa Victoria kabla mambo hayajaharibika. Kuharibiwa kwa chanzo hiki muhimu cha maji ni kuhatarisha maisha ya mamilioni ya watu. Tunahitaji kuchukua hatua za dharura ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaoathiri mno ziwa hilo na wote wanaolitegemea kupata mapato," alisema Juliette Biao Koudenoukpo, Mkurugenzi na Mwakilishi wa UNEP wa ukanda wa Afrika.

Ziwa Victoria, linalopita kati ya nchi 3 na eneo lililo na idadi ya zaidi ya watu milioni 40 , umeendelea kupata shinikizo kutokana na usimamiaji mbaya wa taka na uchafuzi ambao umeathiri vibaya afya ya wanajamii na kuhatarisha uwepo wa ziwa hilo.  Utafiti uliofanywa kwenye fukwe zinazopatikana eneo la kusini ulidhibitisha kuwa kuna plastiki kwenye asilimia 20 ya samaki. Ijapokua tatizo hili ni kuu, kiwango kamili cha uchafuzi huu hakijabainika, huku kukiwa na kiwango kidogo mno cha utafiti kwenye mfumo huu muhimu wa ekolojia.

Safari hiyo inaenda sambamba na wito unaotolewa kwa nchi zote Wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki kukubaliana kama kanda na kuwa mstari mbele kutunga sheria za kukabiliana na matumizi ya plastiki na kukomesha matumizi ya plastiki isiyohitajika inayotumika tu mara moja.

"Kama mhusika kutoka ukanda huu anayejishughulisha na kutunza mfumo wa ekolojia wa Ziwa Victoria, ni vyema kwa AFD kuunga mkono safari hii ya kipekee," alisema Christian Yoka, Mkugenzi wa AFD wa Ukanda wa Afrika Mashariki. "Tumekuwa tukishirikiana kufanya kazi na wadau wetu kutoka Kenya, Uganda na Tanzania ili kupata suluhisho la kipee ili kuwezesha jamii zinazoishi karibu na Ziwa Victoria kupata maji safi na kutunza rasilimali kupitia utafiti na kuwekeza ipasavyo kwenye miundo msingi ya usafi. Tunaamini kuwa masuluhisho yatakayowezesha kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu yanahitaji ushirikiano na juhudi za pamoja zitakazochukuliwa kwa kiwango kinachohitajika.

Safari ya Flipflopi kwenye Ziwa Victoria:

  • Itaonyesha athari za vichafuzi katika mazingira ya ziwa na afya ya binadamu.
  • Itafundisha jamii umuhimu wa kutegemea uchumi wa jadi kwa kutumia vitu vilivyotumika awali kuunda bidhaa na kanuni kuhusiana na vichafuzi viwe vya plastiki au la kwa kuwaelimisha na kuwapa fursa ya kueleza kuhusu wanayoyafahamu.
  • Itawezesha kuwa na maonyesho ya vitu vilivyobuniwa na wenyeji wa eneo hilo.

Mashua, itakayofika Kisumu, mji unaopatikana karibu na ziwa nchini Kenya, itahifadhiwa na KWS kwenye Mbuga ya Impala inayopatikana karibu na Ziwa Victoria. Wakazi wa eneo hilo wanaalikwa kutembelea Flipflopi na kujielimisha kuhusu historia yake, lengo lake, na nia ya kufanya safari katika Ziwa Victoria. Watoto wanashauriwa kushiriki ili wajifunze kuhusu uchafuzi wa hewa na kuwawezesha kushiriki kwenye vita dhidi ya uchafuzi wa plastiki katika jamii zao na kuvuka mipaka ya jamii zao.

"Tumefurahi kufanikisha safari ya Flipflopi ili kukabiliana na uchafuzi wa plastiki nchini na kwenye eneo hili" alisema Edwin Wanyonyi, Mkurugenzi wa Mkakati na Mabadiliko wa KWS. "Ushirikiano huu na kuhifadhi mashua ya Flipflopi kwenye majengo yetu ni ishara tosha kuwa tumejitolea kutekeleza marufuku ya matumizi ya plastiki inatumiwa tu mara moja katika maeneo yetu yaliyohifadhiwa. Safari inaendelea kuonyesha kile tunachoweza kufanya na yale tunayoweza kutekeleza iwapo tutashirikiana" aliongezea.

Ili kusherehekea kuzinduliwa kwa safari ya Flipflopi kwenye Ziwa Victoria, filamu fupi iliyofadhiliwa na UNEP na kutolewa kupitia Flipflopi, iliyoandikwa na kusimuliwa na mwigizaji mtajika nchini Kenya John Sibi-Okumu ikiendeshwa na mshindi wa tuzo la uhuishaji Kwame Nyong’o, ilionyeshwa tarehe 17 Septemba wakati wa kuadhimishwa kwa 'World Clean-Up', vuguvugu la uraia linalohimiza ukusanyaji wa uchafu na taka isiyoshughulikiwa vizuri kutoka katika fukwe zetu, mito yetu, misitu yetu na kwenye barabara zetu. Ikilenga kuwafundisha watoto, filamu hiyo inahadithia jinsi Flipflopi ilivyotengenezwa, na lengo lake.

Dkt. Amina Mohamed, Waziri wa Michezo, Turathi na Utamaduni nchini Kenya tayari ameeleza kuwa ana matumaini baada ya kufahamishwa kuhusu kinachoendelea: "Huu ni mradi mzuri. Unaleta maendeleo na ninajivuna kwa sababu ulibuniwa nchini Kenya."

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Pia tazama wito unaotolewa kwa ukanda kukomesha matumizi ya plastiki inayotumiwa tu mara moja

Kuhusu Flipflopi

Flipflopi ni boti ya ya kwanza duniani iliyotengenezwa kutoka kwa uchafu wa plastiki tu na ndara zilizokusanywa ufukweni na mijini katika pwani ya Kenya. Flipflopi ilizungumziwa na vyombo vya habari duniani 2019 iliposafiri umbali wa kilomita 500 kutoka Lamu, nchini Kenya hadi Zanzibar, nchini Tanzania kama sehemu ya mradi wa UNEP wa 'Clean Seas', kuhamasisha jamii za kimataifa kuhusu athari za uchafuzi wa plastiki ili kubadili mienendo na tabia zinazohusiana na uchafu wa plastiki.

Safari mpya imepangwa kutokea mwezi wa Januari mwaka wa 2021 katika Ziwa Victoria, ziwa kubwa mno la maji safi barani Afrika, na eneo linalokaliwa na watu milioni 40. Safari hii inalenga kuhamasisha ulimwengu kuhusu uchafuzi unaoathiri afya ya watu na mazingira ya ziwa hilo, na kushirikisha jamii, mashirika ya biashara na watungasera nchini Uganda, Tanzania na Kenya kujitolea kukomesha matumizi ya plastiki inayotumiwa tu mara moja. Maono ya Flipflopi ni kuwa na dunia iliyopika marufuku matumizi ya plastiki inayotumiwa tu mara moja, na kuhimiza kuwepo na uchumi ambapo uzalishaji na matumizi ya bidhaa za plastiki zinazoweza kutumiwa zaidi ya mara moja.

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)
UNEP in mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira.  Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.

Kuhusu Kampeni ya UNEP ya Clean Seas
Kampeni iliyozinduliwa mnamo Februari mwaka wa 2017, Kampeni ya Clean Seas  ni mradi unaoshirikiana na serikali, mashirika ya biashara na wananchi kwa lengo la kokomesha matumizi ya plastiki inayotumika tu mara moja na kuwezesha kutunza bahari na mito yetu. 

Kufikia sasa, nchi 60 kote ulimwenguni zimejiunga na kampeni hiyo. Kujitolea kwa nchi wanachama kumefikia zaidi ya asilimia 60 ya nchi zilizo na pwani duniani. Nchi nyingi zimetoa ahadi ya kupunguza au kukomesha matumizi ya plastiki inayotumika tu mara moja katika jamii, au kuwekeza zaidi ili kuunda bidhaa zinatokana na plastiki.

Kuhusu Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD)
Agence Française de Développement (AFD) hutoa ufadhili kwa umma ili kukuza na kuwezesha dunia kuwa na haki na maendeleo endelevu. Kama shirika linalotoa misaada nje ya nchi ili kuwezesha maendeleo endelevu na kufanya uwekezaji, sisi na wabia wenza hushirikiana kupata masuluhisho, kwa ushirikiano na kwa manufaa ya watu walio Kusini mwa dunia.

Vikosi vya AFD vinajishughulisha na miradi zaidi ya 4,000 nyanjani - kwenye nchi nje ya Ufaransa zilizo chini ya Ufaransa na nchi zinginezo 115. Wanalenga kukuza afya, elimu na usawa wa jinsia, na wanafanya kazi kutunza rasilimali zinazomilikiwa kwa pamoja — amani, bayoanuai, na mazingira dhabiti.

Kuhusu World Cleanup Day

World Cleanup Day, iliyoandaliwa mwaka wa 2020 tarehe 19 Septemba, ni mradi unaotokea mara moja kwa mwaka katika jamii duniani kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya taka ya mango duniani, ikijumuisha uchafu baharini. Siku ya Kufanya Usafi Duniani huadhimishwa kwa kukusanya taka na shughuli za kushughulikia taka katika maeneo mbalimbali duniani.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:

Mohamed Atani, Msimamizi wa Mawasiliano n Uhamasishaji Barani Afrika, UNEP,

Caroline Kiiru, The Flipflopi Expedition,