Picha: MAJDI FATHI / NurPhoto / NurPhoto kupitia AFP
30 Mar 2023 Toleo la habari Kushughulikia kemikali na uchafuzi

Maadhimisho ya Kwanza ya Siku ya Kimataifa ya Kutozalisha Taka Kabisa yanaimarisha juhudi za kukabiliana na janga la uchafuzi duniani

Picha: MAJDI FATHI / NurPhoto / NurPhoto kupitia AFP

Nairobi, Machi 30, 2023 – Ili kukabiliana na athari mbaya za taka kwa afya ya binadamu, kwa uchumi na kwa mazingira, dunia leo iliadhimisha kwa mara ya kwanza Siku ya Kimataifa ya Kutozalisha Taka Kabisa, ambayo inahimiza kila mtu kuzuia na kupunguza taka na kuwezesha jamii kuwa na uchumi unaotumia bidhaa tena na tena.

“Janga la taka linadhoofisha uwezo wa Dunia wa kuwezesha maisha. Taka hugharimu uchumi duniani mabilioni ya dola kila mwaka,” Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema kupitia ujumbe wa video kuhusu Siku hii. “Kwa kutumia mazingira kama dambo, tunajichimbia makaburi yetu wenyewe. Ni wakati wa kutafakari kuhusu madhara ya taka kwa sayari yetu - na kutafuta masuluhisho kwa hatari hii mbaya kabisa."

Siku iliyooanzishwa kupitia azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kufuatiwa na maazimio mengine kuhusu taka, ikiwa ni pamoja na ahadi za Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa za tarehe 2 Machi, mwaka wa 2022 za kuendeleza makubaliano ya kimataifa ya kukomesha uchafuzi wa plastiki, Siku ya Kimataifa ya Kutozalisha Taka Kabisa inaendeshwa kupitia ushirikiano wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Shririka la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat).  Siku hii inatoa wito kwa washikadau wote - ikijumuisha serikali, mashirika ya uraia, mashirika ya biashara, wasomi, jamii, wanawake na vijana - kushiriki katika shughuli zinazohamasisha kuhusu miradi ya kutozalisha taka kabisa.

Binadamu huzalisha zaidi ya tani bilioni 2 za taka mango ya manispaa kila mwaka, ambayo sehemu yake ya asilimia 45 haishughulikiwi ipasavyo. Bila hatua za dharura kuchukuliwa, hii itaongezeka hadi takribani tani bilioni 4 kufikia mwaka wa 2050. Taka huwa za aina mbalimbali na kiwango chochote - ikiwa ni pamoja na plastiki, uchafu kutoka kwa uchimbaji madini na maeneo ya ujenzi, vifaa vya elektroniki na chakula.  Huathiri vibaya maskini, na hadi watu bilioni 4  hukosa kufikia vifaa vinavyodhibitiwa vya kutupa taka.

Siku ya Kimataifa ya Kutozalisha Taka Kabisa inalenga kuangazia athari hizi nyingi za taka duniani na kuhimiza hatua za kimataifa katika viwango vyote za kupunguza uchafuzi na taka.

"Kushughulikia taka ni muhimu ili kukabiliana na changamoto za makazi, jinsi tunavyoshughulikia usafi katika miji yetu na janga la mabadiliko ya tabianchi hasa, alisema Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Habitat Maimunah Mohd Sharif. "Ni muhimu ili kuboresha maisha ya watu popote walipo."

Katika azimio lake la kuanzisha Siku hii, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilisisitiza kuhusu umuhimu wa miradi ya kutozalisha taka na kutoa wito kwa washikadau wote kushiriki katika "shughuli zinazolenga kuhamasisha kuhusu miradi katika ngazi ya kitaifa, maeneo katika taifa, ya kikanda na ya eneo na mchango wake ili kufikia maendeleo endelevu”. 

Kukuza miradi ya kutozalisha taka kunaweza kusaidia kuendeleza malengo yote na shabaha za Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu, ikijumuisha Lengo la 11 la Maendeleo Endelevu la kufanya miji na makazi ya watu kuwa jumuishi, salama, thabiti na endelevu na Lengo la 12 la Maendeleo Endelevu la kuhakikisha kuna ruwaza ya matumizi na uzalishaji endelevu wa bidhaa.

"Tunahitaji kuchukua hatua sasa," Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Inger Andersen alisema. "Tuna utaalamu wa kiufundi na msukumo wa kufanya uvumbuzi. Tuna maarifa - yawe ya kisayansi au maarifa ya kiasili - ya kupata masuluhisho kwa janga la taka. 

"Siku ya Kimataifa ya Kutozalisha Taka Kabisa ni fursa halisi ya kukukuza miradi ya eneo, kikanda na kitaifa ya kuimarisha ushughulikiaji wa taka unaojali mazingira na kuchangia katika Malengo ya Maendeleo Endelevu," aliongeza.

Türkiye, ambayo ilizungumza kuhusa azimio hilo na kuungwa mkono na nchi nyingine 105, iko msitari mbele kwa vuguvugu la kutozalisha taka kabisa. Türkiye ilizindua mradi wake wa kutozalisha taka kabisa katika mwaka wa 2017 chini ya uongozi wa Mheshimiwa Emine Erdoğan, Mke wa Rais. Wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika mwaka wa  2022, Mke wa Rais wa Türkiye na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa walitia sahihi hati ya nia njema ya kupanua mradi wa kutozalisha taka kabisa kote duniani. 

"Mradi wa Kutozalisha Taka Kabisa, tuliouzindua miaka mitano iliyopita, ni hatua muhimu ya kuchukua hatua za kuitikia wito wa mazingira wa kuomba msaada," Mheshimiwa Emine Erdoğan alisema. "Mradi wa Kutozalisha Taka Kabisa umekua miaka inaposonga - mtu kwa mtu, jiji kwa jiji na kanda kwa kanda - na kuwa vuguvugu la kimataifa lililoenea nje ya mipaka ya nchi yetu.  Ninaamini kuwa tarehe hii ya leo itakuwa mwanzo wa siku bora zaidi duniani, makazi yetu ya pamoja.”

Kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutozalisha Taka Kabisa, mashirika ya biashara, serikali, mashirika yasiokuwa ya biashara na wengineo wanaandaa hafla kote duniani. Zinajumuisha vikao vya kutoa taarifa kwa jamii, hafla za ukusanyaji wa taka za kielektroniki na taka ya chakula, maonyesho ya mitindo, maonyesho ya picha na makongamano.  

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ataitisha mkutano wa ngazi ya juu mjini New York ili kutoa jukwaa la kubadilishana uzoefu na masimulizi ya mafanikio ya Nchi Wanachama katika kuendeleza na kutekeleza masuluhisho na teknojia ya kushughulikia taka mango. 

UNEP, ikiwa ni pamoja na kupitia Mtandao wake wa Sayari Moja na UN-Habitat itafanya kampeni na juhudi za pamoja za kuwafikia watu katika maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kutozalisha Taka Kabisa tarehe 30 Machi kila mwaka ili kuendelea Kutafuta kuuungwa mkono na kuchukua hatua kutokana na umuhimu wa kutozalisha taka kabisa.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Siku ya Kimataifa ya Kutozalisha Taka Kabisa

Siku ya Kimataifa ya Kutozalisha Taka Kabisa, inayoadhimishwa kwa mara ya kwanza tarehe 30 Machi 2023 chini ya usimamizi wa UNEP na UN-Habitat, inalenga kuhamasisha kuhusu umuhimu wa kutozalisha taka na kukuza mazoea ya uzalishaji na matumizi ya bidhaa kwa njia ya kuwajibika na ushughulikiaji wa taka mijini unaochangia katika kufikia maendeleo endelevu. Siku hii inatoa wito wa kutafakari kuhusu mienendo yetu na kukumbatia uchumi unaotumia bidhaa tena na tena, hali inayomaanisha kupunguza matumizi ya rasilimali na uzalishaji wa hewa chafu kwa mazingira katika hatua zote za mzunguko wa bidhaa, kama sehemu muhimu ya kushughulikia changamoto za aina tatu duniani za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na uchafuzi, na kufanya sayari na binadamu kuwa na afya na kustawi.

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.    

Kuhusu Shririka la Makazi la Umoja wa Mataifa

UN-Habitat ni taasisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na ukuzaji endelevu wa miji. Ina programu katika zaidi ya nchi 90 zinazosaidia watunga sera na jamii kuunda miji endelevu inayojali jamii na mazingira. UN-Habitat inakuza mabadiliko chanya katika miji kupitia maarifa, ushauri wa kisera, msaada wa kiufundi na hatua za ushirikiano.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:

Kitengo cha Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa

Kitengo cha Habari na Vyombo vya Habari, UN-Habitat