Credit: UNEP/Ollivier Girard
05 Jun 2023 Toleo la habari Kushughulikia kemikali na uchafuzi

Siku ya Mazingira Duniani inaangazia masuluhisho kwa uchafuzi wa plastiki

Abidjan, Juni 5, 2023 - Watu binafsi, jamii, mashirika ya uraia,mashirika ya biashara, na serikali kote ulimwenguni leo waliadhimisha Siku ya Mazingira Duniani wakiangazia masuluhisho kwa uchafuzi wa plastiki, huku maadhimisho rasmi yakiandaliwa mjini  Abidjan, nchini Côte d’Ivoire, kwa ushirikiano na Uholanzi. Kuangazia masuluhisho kwa uchafuzi wa plastiki wakati wa  maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ni muhimu, hasa baada ya kuitimika kwa awamu ya pili ya mazungumzo kuhusu makubaliano ya kimataifa ya kukomesha uchafuzi wa plastiki nchini Ufaransa.

Mwaka wa 2023 ni maadhimisho ya miaka 50 ya Siku ya Mazingira Duniani, tangu ilipozinduliwa na Baraza la Umoja wa Mataifa katika mwaka wa 1972. Kwa kipindi cha miongo tano iliopita, chini ya usimamizi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), siku hii imekua na kuwa mojawapo ya majukwaa makubwa zaidi duniani yanayohamasisha kuhusu masuala ya mazingira. Mamilioni ya watu hushiriki kupitia mtandaoni na kupitia shughuli, hafla na kuchua hatua nyanjani kote ulimwenguni.

"Plastiki hutengenezwa kutoka kwa fueli ya visukuku – jinsi tunavyozalisha plastiki zaidi ndivyo tunapotumia nishati ya visukuku zaidi, na ndivyo tunavyozidisha madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Ila tuna masuluhisho,” Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema katika ujumbe wake wa Siku ya Mazingira Duniani. “Ni sharti tushirikiane kama – serikali, makampuni, na watumizi wa bidhaa – kukabiliana na mazoea yetu ya kutumia plastiki, kupigania kutozalisha taka kabisa, na kukuza uchumi unaotumia bidhaa tena na tena.”

Akizungumza katika hafla rasmi ya Espace Latrille Events Deux Plateaux mjini Abidjan, Bw. Jean-Luc Assi, Waziri wa Côte d’Ivoire wa Mazingira na Maendeleo Endelevu, alisema: "Côte d'Ivoire ilitoa amri mwaka wa 2023 ya kupiga marufuku uzalishaji, uagizaji na uuzaji, umiliki na matumizi ya mifuko ya plastiki. Imesaidia mashirika ya biashara kuhamia kwa mifuko inayoweza kutumika tena na inayoweza kuoza. Jiji kubwa zaidi nchini la Abidjan, pia limekuwa kitovu cha mashirika yanayoanza yanayokabiliana na uchafuzi wa plastiki. Wanatiwa moyo. Kwa hivyo ni vyema kufahamu umuhimu wa kukabiliana na uchafuzi wa plastiki. Tuchukue hatua sasa na sote tuseme la kwa uchafuzi wa plastiki.

Siku ya Mazingira Duniani inasaidia kuangazia changamoto zinazotukabili kwa sasa. Changamoto kama vile mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa bayoanuai, na uchafuzi. Uchafuzi wa plastiki unahusiana na changamoto zote tatu zilizotajwa,” alisema Vivianne Heijnen, Waziri wa Uholanzi wa Mazingira. “Ni muhimu kuendelea kuhamasisha, kutumia mbinu bora zaidi, na kuhakikisha kila mshikadau anawajibika. Ni matumaini yangu kuwa Siku ya Mazingira Duniani itazidi kuwa hafla kuu katika ushirikiano wetu wa kukomesha uchafuzi wa plastiki.”

Binadamu hutengeneza zaidi ya tani milioni 430 za plastiki kila mwaka, thuluthi mbili ni vitu visivyodumu ambavyo hufanywa taka baada ya muda mchache. Na gharama kwa jamii na kwa uchumi za uchafuzi wa plastiki ni kati ya Dola za Marekani bilioni 300 na bilioni 600 kwa mwaka. Kwa mjibu wa ripoti ya hivi karibuni ya UNEP, Kukomesha Mtiririko, Uchafuzi wa plastiki unaweza kupunguzwa kwa asilimia 80 kufikia mwaka wa 2040 iwapo nchi na kampuni zinaweza kuweka sera thabiti na mabadiliko ya soko kwa kutumia teknojia iliopo.

"Kwa ajili ya sayari thabiti, kwa ajili ya afya yetu, kwa ajili ya ustawi wetu, ni sharti tukomeshe uchafuzi wa plastiki. Hii itahitaji kuzingatia upya jinsi tunavyozalisha, kutumia, kurejesha na kutupa plastiki na bidhaa zilizotumiwa kuitengeneza,” alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa (UNEP). “Jinsi dunia inavyotengeneza, kutumia na kutupa plastiki imepelekea kuwepo na janga. Lakini ni hali tunayoweza kuepuka kwa kukomesha Mtiririko wa uchafuzi wa plastiki. Wakati wa Siku ya Mazingira Duniani, natoa wito kwa kila mtu kujiunga na vuguvugu la kimataifa. Na kutusaidia kukomesha uchafuzi wa plastiki, kabisa.

Na awamu ya pili ya Kamati ya Majadiliano ya Serikali Mbalimbali (INC) kuhusu uchafuzi wa plastiki mjini Paris, Ufaransa, mwenyekiti wa INC alipewa mamlaka ya kuandaa makubaliano ya kisheria ya kimataifa kuhusu uchafuzi wa plastiki, ikiijumuisha mazingira ya maeneo ya bahari.

Februari mwaka wa 2022, wakati wa kikao cha tano cha Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa  (UNEA-5.2), azimio la kihistoria (5/14) lilipitishwa ili kuunda chombo cha kisheria cha kimataifa kuhusu uchafuzi wa plastiki, ikijumuisha katika mazingira ya baharini na lengo la kukamilisha mazungumzo hayo kufikia mwishoni mwa mwaka wa 2024. Chombo hicho kinapaswa kuzingatia mbinu pana inayokabiliana na mzunguko mzima wa plastiki. Kikao cha tano cha INC kitafinyika mjini Nairobi, nchini Kenya katika mwezi wa Novemba mwaka wa 2023.

Hatua za kushughulikia uchafuzi wa plastiki

Kote duniani, kuelekea na hata Siku ya Mazingira Duniani, kasi ya juhudi duniani iko wazi. Ramani hii ya Siku ya Mazingira Duniani inaonyesha masuluhisho yaliovumbuliwa na jamii kupunguza uchafuzi wa plastiki. Mamia ya shughuli zimesajiliwa, kuanzia kwa usafishaji wa fukwe nchini Mumbai hadi kwa ushonaji wa begi nchini Ghana na tamasha la kutozalisha uchafuzi wa plastiki mjini Atlanta.

Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga na UNEP walitangaza Mkataba wa Maelewano, unaowiana na Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya 2030 ya Maendeleo Endelevu, ili kushughulikia changamoto za uendelevu katika sekta ya anga. Kupunguza matumizi ya bidhaa za plastiki inayosababisha matatizo inayotumika mara moja na kuboresha mzunguko wa matumizi ya plastiki na sekta ya anga ni lengo kuu la ushirikiano.

Katika hafla ya Siku ya Mazingira Duniani katika Mkutano wa Kilele wa Kimataifa wa Usafiri wa Umma wa Duniani wa Muungano wa Kimataifa wa Usafiri wa Umma (UITP), mjini Barcelona, nchini Uhispania, UNEP na UITP walizindua Mkataba wa Maelewano ili kufanya ushirikiano wao kuwa rasmi, kwa kuzingatia sana uhamasishaji wa mazingira na uendelevu katika mitandao ya usafiri wa umma.

Kwa msaada wa UNEP, Jyrgalan, kijiji katika Jamhuri ya Kyrgyz, hivi karibuni kilizindua kituo chake cha kwanza cha kukusanya taka; kituo kinacholenga kushughulikia changamoto za taka zinazoongezeka katika kijiji hicho- zinazosababishwa na kuongezeka kwa utalii - kupitia kujengea uwezo mashirka madogo ya biashara na kuimarisha nafasi ya wanawake katika kufanya maamuzi.

Nchini Panama, chini ya uongozi wa wawakilishi wa UNEP wa serikali ya Panama, ofisi za Umoja wa Mataifa katika ngazi ya kikanda na kitaifa na mashirika ya uraia, ikiwa ni pamoja na mashirika ya vijana, waliahidi kupunguza taka za plastiki katika ofisi zao na jamii zao.   

Nchini Ugiriki, kutokana na mafunzo kutoka kwa shirika lisilo la shirika lisilo la biashara la Enaleia, wavuvi kutoka bandari 42 wameacha kutupa takataka na badala yake kuondoa plastiki baharini kwa kutumia nyavu zao.  Lilianzishwa kwa ushirikiano na Lefteris Arapakis, Kijana Bingwa Duniani wa UNEP kutoka Ulaya, Enaleia hivi majuzi  lilitangaza kwamba sasa litaanza kufanya kazi nchini Misri na Uhispania na kuimarisha juhudu zake nchini Kenya na Italia.

Mkataba wa Plastiki wa Kenya ulitoa mwongozo mpya kwa viwanda kuhusu uchakataji wa mifuko ya plastiki. Mwongozo huo unalenga kutoa mapendekezo ya wazi kwa wafanya maamuzi kuhusu jinsi ya kuunda mifuko ya plastiki ili kuendana na miundomsingi ya mitambo ya kuchakata.

Mjini New York, mradi wa sanaa uliotengenezwa kwa taka za plastiki pekee utazinduliwa katika Kituo cha Biashara cha Ulimwenguni. Nchini India, wasanii nyota na wanamuziki maarufu wamekusanyika ili kuunda video ya muziki na kushiriki jumbe za kuhimiza watu zaidi kuchukua hatua dhidi ya uchafuzi wa plastiki. Nchini Kazakhstan, kikundi cha muziki nchini cha Great Steppe kilitoa video ya muziki kuadhimisha Siku hiyo na kuangazia madhara ya mazingira yanayokabili Bahari ya Aral, huku hafla ya mitindo na sanaa endelevu inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa mjini Almaty ikionyesha sanaa kutoka kwa nyenzo zilizochakatwa. 

Viwanja vya ndege na mitandao ya usafiri kote ulimwenguni, kuanzia China na Indonesia hadi Chile na Marekani, pamoja na mabango katika Times Square na Piccadilly Circus yalitangaza jumbe za Siku ya Mazingira Duniani, na kuhamasisha mamilioni ya abiria na wananchi kuhusu umuhimu wa hatua za kukabiliana tishio la uchafuzi wa plastiki.

Maelfu ya watu waliadhimisha Siku ya Mazingira Duniani mtandaoni, wakitumia hashtagi za siku hiyo #SikuYaMazingiraDuniani na #KomeshaUchafuziWaPlastiki zilizovuma katika nambari moja na mbili mtawalia kwenye Twitter.  Zaidi ya watu 50,000 walipakua Mwongozo wa Vitendo wa UNEP wa Kukomesha Uchafuzi Wa Plastiki.

Hafla, matukio, hatua na maonyesho haya, yaliyofanyika katika vituo vya jamii, shule, mashirika ya biashara na nyumbani, hali inayoonyesha jinsi watu binafsi na jamii ni vichochezi muhimu vya hatua za kushughulikia mazingira.  Wanaweza kuchochea serikali, miji, taasisi za fedha na viwanda kutumia uwezo wao kuwekeza na kutekeleza masuluhisho makubwa ili kukomesha na kukabiliana na janga la uchafuzi wa plastiki.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Siku ya  Mazingira Duniani

Siku ya Mazingira Duniani tarehe 5 Juni ni mojawapo ya siku kuu ya kimataifa yamazingira. Ikiongozwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na inayoadhimishwa kila mwaka tangu mwaka wa 1973, hafla hii imekua na kuwa jukwaa kubwa zaidi duniani la kuhamasisha kuhusu mazingira, huku milioni ya watu kutoka pembe zote za dunia wakishiriki ili kutunza sayari yetu.

 

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano wa kutunza mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.

 

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:    

Kitengo cha Habari na Vyombo vya Habari cha Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa

*Makala haya yalisasishwa Juni 6, 2023 ili kutumia jina sahihi la Muungano wa Kimataifa wa Usafiri wa Anga (IATA)