Naja Bertolt Jensen/Unsplash
21 Oct 2021 Toleo la habari Kushughulikia kemikali na uchafuzi

Tathmini kamili kuhusu uchafu wa baharini na uchafuzi wa plastiki inaonya dhidi ya masuluhisho bandia na kuthibitisha kuna haja ya kuchukua…

Nairobi, 21 Oktoba 2021 - Kupunguza kwa kasi kwa plastiki isiyohitajika, inayoweza kuepukika na inayosumbua ni muhimu ili kushughulikia janga la plastiki duniani, kwa mjibu wa tathmini kamili iliyotolewa leo na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).  Mabadiliko ya kasi kutoka matumizi ya mafuta ya visukuku hadi matumizi ta nishati jadidifu, kuondolewa kwa ruzuku na mabadiliko kuelekea njia zinazotegemeana ni mambo yatakayosaidia kupunguza taka za plastiki kwa kiwango kinachohitajika.

Kutoka Uchafuzi hadi Kupata Suluhu: tathmini ya kimataifa ya uchafu wa baharini na uchafuzi wa plastiki inaonyesha kuwa kuna tishio linalozidi kuongezeka katika mifumo yote ya ekolojia kuanzia kwa vyanzo hadi baharini.  Inaonyesha pia kuwa ijapokuwa kuna ujuzi, tunahitaji utashi wa kisiasa na hatua za dharura kutoka kwa serikali ili kukabiliana na changamoto zinazoongezeka.  Ripoti hiyo itaongoza majadiliano katika Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA 5.2) katika mwaka wa 2022, ambapo nchi zitakutana kuamua njia za kuwezesha ushirikiano wa kimataifa.

Idadi ya uchafu wa plastiki inayoingia kwenye mifumo ya ekolojia ya majini imeongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni na inakadiriwa kuongezeka maradufu kufikia mwaka wa 2030. Hali itakayosababisha madhara makubwa kwa afya ya binadamu, kwa uchumi duniani, kwa bayoanuai na kwa hali ya hewa.

Tathmini, iliyotolewa siku 10 tu kabla ya COP26, inasisitiza kuwa plastiki ni changamoto kwa mazingira pia:  Kwa kuzingatia kudumu kwake, uzalishaji wa gesi ya ukaa kutoka kwa plastiki katika mwaka wa 2015 ulikuwa gigatani 1.7 za CO2 sawa na (GtCO2e), na inakadiriwa kitaongezeka hadi takriban GtCO2e 6.5  kufikia mwaka wa 2050, au asilimia 15 ya bajeti ya kaboni duniani. ​​

Waandishi wanatashwishi kuhusu kutumia tena na tena plastiki hadi kukomesha janga la uchafuzi wa plastiki. Wanaonya dhidi ya madhara ya vibadala vya plastiki inayotumika mara moja tu na bidhaa zingine za plastiki, ambavyo tayari ni tishio kutokana kemikali sawa na iliyo kwa plastiki za kawaida. 

Ripoti hiyo inaangalia makosa makuu sokoni, kama vile bei nafuu ya mafuta ya visuku yasiyosafishwa ikilinganishwa na vifaa vinavyotengenezwa kutoka kwa plastiki iliyotumika, juhudi zisizokuwa na utaratibu maalum katika ushughulikiajii usio rasmi na rasmi wa taka za plastiki, na ukosefu wa makubaliano kuhusu masuluhisho ya kimataifa.

"Tathmini hii inatoa hoja dhabiti zaidi ya kisayansi kufikia sasa kuhusu udharura wa kuchukua hatua, na juhudi za pamoja za kutunza na kuboresha bahari zetu kuanzia vyanzo hadi baharini," alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP.  "Wasiwasi mkuu unahusu hatima ya bidhaa zinazooza, kama vile chembechembe za plastiki na kemikali zinazoongezwa, ambazo nyingi huwa na sumu, na ni hatari kwa afya ya binadamu, kwa wanyamapori, na kwa mifumo ya ekolojia.  Kasi ambayo uchafuzi wa plastiki baharini unashika makini ya umma ni hali inayotia moyo.  Ni muhimu kutumia kasi hii kutilia manani fursa za kuwa na bahari safi, iliyo kwenye hali nzuri na dhabiti. ”

Ripoti hii inaonyesha kwamba plastiki huchangia asilimia 85 ya takataka za baharini na inaonya kuwa kufikia mwaka wa 2040, kiwango cha uchafu wa plastiki katika maeneo ya baharini kitaongezeka karibu mara tatu, na kuongeza tani milioni 23-37 za taka ya plastiki baharini kila mwaka.  Hii inamaanisha takribani kilo 50 za plastiki kwa kila mita ya ukanda wa pwani kote ulimwenguni.

Kwa hivyo, viumbe wote baharini - kuanzia kwa planktoni na samakigamba hadi kwa ndege, kobe na mamalia - wamo hatarini mno kudhuriwa na sumu, mienendo isiyofaa, njaa na ukosefu wa hewa.  Matumbawe, mikoko na nyasi baharini pia huathiriwa na taka za plastiki zinazovizuia kupata oksijeni na mwangaza. 

Mwili wa binadamu vilevile unaweza kudhuriwa kwa njia mbalimbali kutokana na uchafuzi wa plastiki kwenye vyanzo vya maji, hali inayoweza kusababisha mabadiliko ya homoni, shida za ukuaji, matatizo ya uzazi na saratani.  Plastiki humezwa kupitia vyakula vya baharini, vinywaji na hata chumvi ya kawaida; hupenya kwenye ngozi na huvutwa inapopatikana hewani.

Takataka za baharini na uchafuzi wa plastiki pia huathiri mno uchumi duniani.  Gharama kwa uchumi kutokana na uchafuzi wa plastiki baharini hasa kuhusiana na athari zake kwa utalii, uvuvi na ufugaji wa samaki, pamoja na gharama zingine kama zile za kukusanya taka, zilikadiriwa kuwa angalau dola za Marekani kati ya bilioni 6 na bilioni 19 kote ulimwenguni katika mwaka wa 2018. Inakadiriwa kuwa kufikia mwaka wa 2040 kunaweza kuwa na hatari ya kifedha ya dola za Marekani bilioni 100 kwa wafanyabiashara ikiwa serikali zitawataka kulipia gharama za kushughulikia taka kutegemea kiwango kinachotarajiwa na uwezo wake wa kutumika tena.  Kiwango kikubwa cha taka za plastiki pia kinaweza kusababisha kuongezeka kwa utupaji haramu wa taka nchini na katika ngazi ya kimataifa.

Tathmini inatoa wito wa kupunguzwa kwa plastiki mara moja na inahimiza mabadiliko katika mfumo mzima wa uzalishaji, uuzaji na matumizi ya plastiki.  Uwekezaji zaidi unahitaji kufanyika kupitia mifumo thabiti na bora zaidi za ufuatiliaji ili kutambua vyanzo, kiwango na hatima ya plastiki na maendeleo ya mfumo wa kutathmini hatari, hali inayokosekana katika kiwango cha kimataifa.  Mwishowe, mabadiliko kwa mbinu za kutumia bidhaa tena na tena, ikijumuisha matumizi na mazoea ya uzalishaji endelevu, maendeleo ya kasi na kupitishwa kwa njia mbadala na mashirika ya biashara na kuimarisha uelewa wa wanunuzi ili wafanye uamuzi mwafaka

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Kampeni ya Bahari Safi

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa lilizindua Kampeni ya Bahari Safi katika mwaka wa 2017 kwa lengo la kukuza vuguvugu la kimataifa la kubadilisha mwelekeo wa plastiki kwa kupunguza matumizi hatari, yasiyohitajika, yanayoweza kuzuilika ya plastiki ikijumuisha plastiki inayotumika tu mara moja na kukomesha chembechembe za plastiki zinazoongezwa kimakusudi. Kutokea hapo, nchi 63 zimetoa ahadi za kuchukua hatua za kuimarisha usimamizi wa taka kupitia kupunguza matumizi ya plastiki inayotumika tu mara moja na kadhalika.  Kampeni hii sasa itaangazia masuala kuanzia vyanzoni hadi baharini na masuluhisho na kutoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za dharura kote ulimwenguni. 

Kampeni hii inachangia malengo ya Ubia wa Kimataifa wa Taka Baharini na Ahadi Mpya za Plastiki Duniani 

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) 

UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira ulimwenguni. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.  

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:

Keisha Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa