UNEP/Todd Brown
15 Apr 2024 Toleo la habari Kutumia mazingira kushughulikia tabianchi

Upendekezaji wa watakaotuzwa Tuzo la Mabingwa wa Dunia la UNEP mwaka wa 2024 umefunguliwa likiangazia uborejeshaji wa ardhi, kustahimili…

  • Tuzo la Mabingwa wa Dunia hutuza watu binafsi na mashirika ambayo huchukua hatua za kusababisha mabadiliko chanya kwa mazingira. 
  • UNEP inatafuta kupendekezwa kwa watu binafsi na mashirika yanayofanya kazi kupata masuluhisho bunifu na endelevu ya kuboresha ardhi, kuimarisha ustahimilivu kwa ukame, na kupambana na kuenea kwa majangwa.
  • Upendekezaji utaanza tarehe 15 April hadi tarehe 5 Mei mwaka wa 2024.

Nairobi, April 15, 2024 – Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) leo limezindua wito wa kupendekeza watakaowania tuzo lake llinalotolewa kila mwaka la Mabingwa wa Dunia – tuzo la Umoja wa Mataifa la ngazi ya juu zaidi linalotolewa kwa heshima ya mazingira ili kujivunia viongozi wa kipekee kutoka kwa serikali, mashirika ya uraia na sekta binafsi kwa mchango wao chanya kwa mazingira.

Mwaka huu, UNEP inahimiza kupendekezwa kwa watu binafsi na mashirika yanayobuni na kutekeleza sera na masuluhisho endelevu ya kuboresha ardhi, kuimarisha ustahimilivu kwa ukame, na kupambana na kuenea kwa majangwa.

Tangu kuzinduliwa kwake katika mwaka wa 2005,  Tuzo la Mabingwa wa Dunia limewatuza washindi 116, ikijumuisha viongozi 27, watu biafsi 70 na mashirika 19. Katika mwaka wa 2023, UNEP ilipokea mapendekezo 2,500, ya wawaniaji wa tuzo hili.

Tunapokaribia nusu ya Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia, hatua za dharura zinahitajika ili kutunza na kuboresha mifumo ya ekolojia.  Uboreshaji wa mifumo ya ekolojia huimarisha maisha, hupunguza umaskini, hukuza ustahimilivu na kupunguza kasi ya janga la mabadiliko ya tabianchi. Ili kusaidia ulimwengu asilia, serikali, mashirika ya uraia na sekta ya kibinafsi ni sharti ziimarishe ufadhili, kujengea uwezo na kubadilisha mienendo.

Siku ya Mazingira Duniani tarehe 5 Juni 2024 itaangazia uboreshaji wa ardhi, kuenea kwa majangwa na kustahimili ukame. Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Majangwa, unaadhimisha miaka kumi na tatu mwaka huu, utaandaa Kongamano la Nchi Wanachama (COP) la kumi na sita katika mwezi wa Desemba.

Kuboresha na kuimarisha mazingira ni muhimu ili kuboresha afya ya binadamu na ya sayari. Viongozi kutoka sekta zote na maeneo yote wanafanya kazi kwa bidii kushughulikia changamoto za aina tatu duniani za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa bayoanuai, na uchafuzi na taka. Mabingwa wa Dunia husaidia kuwa mstari mbele kupigania mambo haya. Wanatukumbusha kuwa uendelevu wa mazingira ni muhimu ili kufikia maendeleo endelevu.

Watu binafsi, mashirika na taasisi za serikali wanaweza kupendekezwa chini ya vitengo vya Uongozi Unaozingatia Sera, Motisha na Kuchukua Hatua, Maono ya Ujasiriamali, na Sayansi na Ubunifu. Upendekezaji wa yeyote na mtu mtu yeyote utaanza tarehe 15 Aprili hadi tarehe 5 Mei mwaka wa 2024. Washindi wa Mabingwa wa Dunia watatangazwa mwishoni mwa mwaka wa 2024.

Pendekeza Bingwa wa Dunia 

Katika mwaka wa 2023, UNEP ilituza watu binafsi, mashirika na serikali zinazotekeleza masuluhisho bunifu ya kukabiliana na uchafuzi wa plastiki. Mabingwa wa Dunia wa mwaka wa 2023 wa UNEP walikuwa:

  • Meya Josefina Belmonte wa Jiji la Quezon, Ufilipino, aliyetuzwa katika kitengo cha Uongozi Unaozingatia Sera, anaendesha juhudi za kujali mazingira na jamii kupitia msururu wa sera za kukabiliana na janga la mabadiliko ya tabianchi, kukomesha uchafuzi wa plastiki na kutochafua maeneo ya miji. Juhudi zake ni pamoja na kupiga marufuku plastiki inayotumika mara moja, mpango wa biashara unaoshughulikia uchafuzi wa plastiki, vituo vya kujaza vitu muhimu vya kila siku na upiganiaji wa uundaji wa sera dhabiti za kimataifa kuhusu plastiki.
  • Wakfu wa Ellen MacArthur (Uingereza), uliotuzwa katika kitengo cha Motisha na Kuchukua Hatua, umetekeleza wajibu mkuu katika kuzingatia mzunguko mzima, ikijumuisha wa plastiki. Wakfu huo umechapisha ripoti na kuanzisha mitandao ya wafanya maamuzi katika sekta ya kibinafsi na ya umma, pamoja na wasomi, ili kukuza mipango na masuluhisho yanayozingatia mzungukuko mzima kwa janga la mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa bayoanuai, uchafuzi wa plastiki na kadhalika. Unaongoza Ahadi za Kimataifa pamoja na UNEP.
  • Blue Circle (China), iliyotuzwa katika kitengo cha Maono ya Ujasiriamali, hutumia teknolojia ya blockchain na mtandao wa mambo kufuata na kufuatilia mzunguko mzima wa uchafuzi wa plastiki - kuanzia kwa ukusanyaji hadi kuunda vitu vipya, kuitengeneza upya na kuiuza tena. Imekusanya zaidi ya tani 10,700 za uchafu kutoka baharini, na kuifanya kuwa programu kubwa zaidi ya Uchina ya taka za plastiki baharini.
  • José Manuel Moller (Chile), aliyetuzwa pia katika kitengo cha Maono ya Ujasiriamali, ni mwanzilishi wa Algramo, shirika la jamii linalojitolea kutoa huduma za kujaza tena vitu vilivyotumika, hali inayopunguza uchafuzi wa plastiki na kupunguza gharama za vitu vinavyotumika kila siku. Moller pia anafanya kazi ya kuzuia, kupunguza na kushughulikia taka kwa njia endelevu kupitia nafasi yake kama Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Umoja wa Mataifa ya Watu Mashuhuri kuhusu kutozalisha taka kabisa, mpango ulioanzishwa Machi mwaka wa 2023.
  • Baraza la Utafiti wa Kisayansi na Viwanda (Afrika Kusini), lililotuzwa katika kitengo cha Sayansi na Ubunifu, hutumia teknolojia ya kisasa na utafiti wa fani mbalimbali kuendeleza uvumbuzi wa kukabiliana na uchafuzi wa plastiki na masuala mengine. Ni mwanzilishi katika kutambua njia mbadala endelevu za kushughulikia plastiki ya kawaida, na kutoa fursa kwa viwanda vya eneo vya kutengeneza bidhaa na kukuza uchumi na kutathini uwezekano wa plastiki kuoza.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Tuzo la UNEP la Mabingwa wa Dunia

Tuzo la UNEP la  Mabingwa wa Dunia hutuza watu binafsi, makundi na mashirika ambayo huchukua hatua za kusababisha mabadiliko chanya kwa mazingira. Tuzo linalotolewa kila mwaka la Mabingwa wa Dunia ni tuzo la Umoja wa Mataifa la ngazi ya juu zaidi linalotolewa kwa heshima ya mazingira. #MabingwaWaDunia

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP in mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.    

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:

Kitengo cha Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa