17 Dec 2019 Tukio Majanga na mizozo

Kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi na uwezekano wa majanga kutokea nchini Mauritius

Taifa la Mauritius ambalo hushuhudia jua kali, taifa lililo na milima ya kuvutia, fukwe za kupendeza na maji tulivu, huvutia watalii wengi. Taifa linalopatikana katika sehemu ya Bahari Hindi ambayo hushuhudia vimbunga vingi, pia lina uwezekano mkubwa wa kuathiriwa vibaya na mabadiliko ya tabianchi. Hali ni mbaya zaidi hadi Ripoti ya Benki ya Dunia ya Kutathmini Uwezekano wa Majanga Kutokea ya Mwaka wa 2018 imeiorodhesha nambari 16 kati ya nchi zilizo na uwezekano mkubwa wa majanga kutokea.

Utalii, ambao ulichangia takribani asilimia 24.3  ya mapato yote ya nchi katika mwaka wa 2018 ikiwa ni ongezeko ikilinganishwa na asilimia 23.8 iliyoshuhudiwa katika mwaka uliotangulia, unaathiriwa kwa kasi kutokana na kuharibiwa kwa matumbawe kutokana na ongezeko la joto baharini na mmomonyoko ufukweni. Kuna baadhi ya fukwe ambazo zimepungua kwa zaidi ya mita 10 katika muongo uliopita.

Nchi hiyo iko hatarini kutokana na majanga mbalimbali ya kimazingira, ya kibayolojia, ya kijiografia na ya kiteknolojia. Katika miaka ya hivi karibuni, kuongezeka kwa kiwango na umaratokezi wa vimbunga, mvua ya masika na mafuriko ya ghafla pia vimehatarisha maisha ya watu kwenye kisiwa hicho.

Mnamo Machi mwaka wa 2013, watu 11 waliuawa na mafuriko ya ghafla katika eneo la Port Louis. Mahali ambapo Kimbunga Fantala cha maeneo ya tropiki, kilichokuwa na kasi ya kilomita 280 kwa saa kilipitia, ilikuwa tishio kwa visiwa vya Agalega na St Brandon vinavyopatikana katika eneo la mteremko.

Mnamo Machi mwaka wa 2017, kutokea kwa Kimbunga Enawo cha maeneo ya tropiki kwa kasi ya kilomita 250 kwa saa katika eneo la Kusini mwa Bahari Hindi ilikuwa tishio kwa kisiwa kikuu cha Mauritius. Hivi karibuni, Mnamo Februari mwaka wa 2017, Kimbunga Gelena kilichokuwa na kasi ya kilomita 165 kwa saa, kilipita katika eneo la takribani kilomita 50 kusini magharibi kwa kisiwa cha Rodrigues na kupelekea mafuriko ya ghafla yaliyosababisha watu 259 kupoteza makazi yao. Pia yaliharibu miundo msingi, maboma binafsi na mashamba na kuathiri mno mfumo wa usambazaji wa nguvu za umeme.

Mfumo wa Mauritius unaotathmini uwezekano wa majanga kutokea Mfumo wa Kimataifa wa Kupunguza na Kukabiliana na Majanga unadokeza kuwa mafuriko yanachukua nafasi ya pili kwa ukubwa kwa kuhatarisha maisha ya watu baada ya vimbunga. Husababisha asilimia 20 ya hasara ya moja kwa moja kwa uchumi kutokana na majanga. Nyingi ya gharama hizi hutokana na kuharibiwa kwa maeneo ya makazi ya binadamu.

Ila, haya yote hayatokani na mabadiliko ya tabianchi. Kuongezeka kwa kasi kwa ujenzi wa miji katika mashamba ya kilimo ni hali inayoweka shinikizo kwa mifumo ya kitaifa ya mabomba ya maji na kusababisha kuongezeka kwa visa vya mafuriko ya ghafla, uharibifu wa nyumba, wa miundo msingi na wa mimea. Hali hii inawaweka watu hatarini kuambikizwa magonjwa yanayotokana na maji.

Ili kukabiliana na kupunguza majanga, katika mwaka wa 2015, nchi ya Mauritius ilianzisha Mpango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Majanga. Mpango huo unajumuisha mfumo mzima wa kukabiliana na majanga, huku ukisisitiza matumizi ya mbinu anuai na kuangazia zaidi uwezekano wa majanga kutokea.

Kutokana na  Tathmini ya Kitaifa Inayotolewa kwa Hiari ya Jukwaa la Kisiasa la Ngazi ya Kiwango cha Juu Kuhusiana na Maendeleo Endelevu, “Mauritius ilisita kuwa nchi ya uchumi wa kipato kidogo na kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha wastani huku ikiwa na lengo la kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha juu licha ya changamoto ilizo nazo kama Taifa Dogo la Kisiwa linaloendelea lisilo na mali ghafi, lisilofikiwa kwa urahisi, ambalo hukumbwa na majanga ya kiasili na kukabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi. Pia limo hatarini mno kuathirika na masuala kutoka mataifa mengine na mienendo ya kimataifa.”

Mnamo Agosti mwaka wa 2019, kutokana na wito wa serikali ya Mauritius, Mradi wa Kuwezesha Kupunguza Majanga ulipeleka kikosi cha wataalamu 11 ili kuwezesha matumizi ya njia anuai kusaidia taifa hilo la kisiwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na athari zinazotokana na majanga. Mradi huo hupokea ufadhili wa kimataifa kutoka kwa mashirika 20 na lengo la kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu kwa kukuza uwezo wa nchi ili kuziwezesha kupunguza athari kwa mazingira na zile zinatotokana na majanga.

“Kuwezesha kuwa na upatikanaji wa miundo misingi ya kupitishia uchafu na ya maji taka ni masuala ya dharura yanayopaswa kushughulikiwa ili kupunguza uwezekano wa majanga kutokea. Hii ni kwa sababu ni asilimia 29 tu ya idadi ya watu wameunganishwa kwa mfumo wa kupitishia taka katika taifa zima. Wengi wao hutumia matangi ya maji machafu ambayo hufurika msimu wa mvua. Kila mafuriko yanapotokea, uwezekano wa kutokea kwa kipindupindu na magonjwa ya tumbo huongezeka,” asema Karin Stibbe mtaalamu wa masuala ya majanga anayefanya kazi na Kikosi cha Pamoja cha Mazingira(JEU) cha Ofisi ya Uratibu ya Masuala ya Misaada na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kupitia kwa Chombo cha Muungano wa Ulaya cha Kulinda raia. Tangu mwaka wa 2014, Mpango huo umetolea JEU wataalamu kama vile Stibbe zaidi ya mara 20.

“Kushughulikia uwezekano wa majanga kutokea kunahitaji ushirikiano. Jamii nchini Mauritius zimejitolea kupunguza uwezekano wa majanga kutokea na serikali imeanzisha kitengo cha polisi cha kushughulikia mazingira ili kuwa cha kwanza kushughulika pale ambapo janga linatokea. Polisi hao wanafanya kazi na Kituo cha Kitaifa cha Kushughulikia na Kupunguza Uwezekano wa Majanga Kutokea. Ijapokuwa sera na taasisi vipo, kuna mwanya katika uratibu na hali hii inaweza kupunguzwa kupitia kushiriki maarifa,” asema Stibbe.

Tangu kuanzishwa kwake katika mwaka wa 1994, Kitengo cha Pamoja cha Mazingira kimetoa wataalamu na vifaa wakati wa dharura zaidi ya mara 200 kote ulimwenguni, kikisaidiwa na mtandao mkuu wa wabia wa kimataifa. Kimeendelea kufanya kazi ili kushughulikia na kukabiliana na madhara kwa mazingira kutokana na majanga yanayotokea ghafla na hali changamano za dharura.

Husaidia nchi kushughulikia kipengee cha mazingira wakati wa majanga yanayohitaji kushughulikiwa kwa dharura kwa kutoa mafunzo kwa wataalamu wanaoweza kutumwa na Umoja wa Mataifa (UN) kushughulikia masuala ya mazingira. Hutoa vifaa na mwongozo kwa wataalamu wa kushughulikia mikasa na wa kushughulikia mazingira ili kutathmini uwezekano wa majanga kutokea, kama vile Vifaa vya Kutathimini Mafuriko ya Ghafla kwa Mazingira na Mwongozo wa Kushughulikia Taka Inayotokana na Majanga.

UNEP pia ni mwanzilishi mwenza wa Ubia wa Mazingira na wa Kupunguza Uwezekano wa Majanga Kutokea, muungano wa kimataifa wa mashirika 24 yanayohimiza masuhuhisho ya kupunguza uwezekano wa majanga kutokea huku yakijali mifumo ya ekolojia. Muungano huo unatoa wito wa uwekezaji zaidi wa kuboresha mifumo ya ekolojia na kuitunza. Kipao mbele hutolewa kwa maziwa, maeneo ya kinamasi na yaliyo na unyevunyevu ili kupunguza madhara yanayotokana na majanga ya maji.

 

Kwa maelezo zaidi kuhusu kazi yetu, tafadhali wasiliana na ochaunep@un.org.

Jifahamishe zaidi kuhusu kazi ya kitengo hiki.

Jifahamishe zaidi kuhusu kazi ya UNEP kuhusu mazingira na matokeo yake wakati wamajanga na mizozo.

 

Maudhui Yanayokaribiana