30 Sep 2019 Tukio Kutumia mazingira kushughulikia tabianchi

Kutilia Maanani Uzalishaji wa Kakao Ulimwenguni

Je wajua kwamba, kwa kawaida, chini ya asilimia 7 ya bei ya kipande chako ya chokoleti huenda kwa wazalishaji wa kakao? Au wingi wa mazao ya kakao duniani yanahusishwa na  ukataji haramu wa miti na uharibifu wa bayoanuai?

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na washirika wake wamekuwa wakifanya kazi pamoja kwa miaka mingi kupitia miradi inayolenga kuifanya sekta ya kakao idumishe utunzaji wa mazingira kwa njia endelevu.

Kutumia mbinu zisizochafua mazingira katika sekta ya kakao ni mojawapo ya miradi hiyo. Lengo lake kuu ni kubadilisha mbinu za uzalishaji na kuweka mazoea azuri ya kibiashara katika nchi kuu zinazozalisha kakao na kampuni za chokoleti kwa madhumuni ya kuhifadhi bayoanuai, kuwa na ustawi mkuu wa muda mrefu kwa wahusika wote na kuongeza mapato kwa wakulima wadogowadogo.

“Shamba letu ni endelevu kwa sababu tuna vitu mbalimbali," asema Clavelina Sanchez katika shamba lake la Nueva Carlifonia lililoko katika idara ya Junin, katika eneo la Selva katikati mwa Peru. “Tuna kahawa, kakao, ndizi, machungwa, achiote, yuca, uncucha,  kuku, mbao na kadhalika.

“Katika uzalishaji wa kakao, shamba letu linatumika kama kielelezo: wakulima wengine huja kupokea mafunzo na kijonea kinachoendelea.  Tunafuata kanuni zetu na kuzitimiza: ukulima endelevu na uzalishaji mseto hutusaidia kuongeza mapato.  Tunatunza bayoanuai na kuboresha maisha yetu.  Kwa mfano tumeonyeshwa (kupitia mradi huu) jinsi ya kutumia miti asili kama kudzu na comelinas kama kivuli na kuzuia mmomonyoko wa udogo.

Lengo letu kuu ni kutunza na kuhifadhi udongo  kwa kutumia mbinu mwafaka. Ni muhimu ili kupata mazao yenye afya yatakayotupa chakula cha kutosha na mapato kwa familia zetu.”

image
Usimamizi bora wa kakao unahusisha kuhifadhi bayoanuai. Picha na Flickr

Kimataifa, mradi huu unahusisha asilimia isiyopungua 10 ya uzalishaji wa kakao ulimwenguni – wakulima 250,000 wanazalisha tani 350,000 za  kakao kwa hekta 750,000 za mashamba. Mradi huu unasaidia kukabiliana na uharibifu wa bayoanuai pamoja na mabadiliko kwa maeneo ya makazi na matumizi mabaya ya ardhi.  Mradi huu pia unaunga mkono mifumo ya usimamizi bora wa kakao inayohifadhi bayoanuai.

“Lengo kuu la kuhusisha uendelevu wa kakao na uhifadhi wa bayoanuai ni umuhimu wake wa kuimarisha mradi," asema  Johan Robinson, mkuu wa kitengo cha UNEP cha Mfuko wa Mazingira Duniani Bayoanuai na Uharibifu wa ardhi .

Matokeo ya Mradi

Matumizi ya Mtandao wa Kilimo Endelevu   kama chombo muhimu cha kukuza uendelevu kwenye mashamba huku bayoanuai ikihifadhiwa ndani na kando ya mashamba hao yamekuwa na ufanisi.

Wakaguzi wa mradi wamethibitisha kwamba mashamba 182,362 yameridhia viwango vya Mtandao wa Kilimo Endelevu. Jumla ya hekta 896, 654 ikiwa ni pamoja na hekta 64,559 ya mashamba ya kilimo yalitengwa ili kuhifadhiwa.  Mradi huu pia umechangia kuhifadhi bayoanuai katika baadhi ya mazingira yaliyochaguliwa kwa ukuzaji wa kakao. Mazingira haya ni kama vile mradi waTai nchini Côte d'Ivoire, mradi wa Juabeso/Bia nchini Ghana, na mradi wa Kanyang nchini Nigeria.

image
Clavelina Sanchez akiwa kwenye shamba lake liliko Nueva California- Peru ya kati. Picha na:  Rainforest Alliance

Shughuli hizi zimeungwa mkono na watengenezaji na wauzaji wa bidhaa zaidi ya 54 walijitolea kudumisha uendelevu.  

Kujitolea huku kwa mashirika kulichangia mno kuwepo na ufadhili wa ziada wa dola za Marekani milioni 24.5 ambazo mradi huu ulipokea. Mawasiliano  kupitia ujumbe ulihamasisha watumizi wa bidhaa na wakulima kuhusu thamani ya vitendo endelevu.   

Mauzo ya kakao  yaliyoidhinishwa ya Rainforest Alliance Certified inawakilisha asilimia 5 ya mauzo kote ulimwenguni. Kando na hayo, kiwango kikubwa cha kakao kinazalishwa kwa njia endelevu ikilinganisha na ile inayouzwa na Rainforest Alliance Certified.

Mtandao wa Kilimo Endelevu/mpango wa kakao wa Rainforest Alliance umeshuhudia ukuaji mkubwa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Katika mwaka wa 2016, takribani hekta milioni moja ya mashamba ya kakao katika nchi 15 zimeridhia viwango vya Mtandao wa Kilimo Endelevu/Rainforest Alliance.  Kwa sasa, kakao iliyoidhinishwa na Mtandao/Alliance ni jumla ya asilimia 13.6 ya kakao inayosambazwa ulimwenguni. Wanunuzi wengi duniani wanaendelea kujitolea kunua kakao inayodumisha uendelevu.

image
Rimberti Prudencio, kiongozi wa jamii, aliyepokea mafunzo ya mradi kama "mkulima mkuu".  Amewaonyesha Sanchez na wakulima wengine wa kiasili jinsi ya kukuza kakao kwa kupitia mbinu endelevu.  Picha na: Rainforest Alliance

Rainforest Alliance, kwa ushirikiano na Wakfu wa Kakao Duniani wametengeneza miongozo  ya ukuzaji wa kisasa unaojali mazingira unaoweza kustahimili hali zote za hewa kwa muda mrefu.

Mradi wa Sekta ya Kakao Usiochafua Mazingira ulianza tangu mwaka wa 2013 hadi 2019 na unafadhiliwa na Mfuko wa Fedha za Mazingira Duniani  na kutekelezwa na UNEP. Unahususha nchi za Brazil, Cote d’Ivore, Jamhuri ya Dominika, Ecuador, Ghana, Guinea, Indonesia, Nigeria, Madagascar, Papua New Guinea na Peru. Mradi huu unaungwa mkono kikamilifu na serikali ya kila nchi husika.

Mshirika mkuu anayetekeleza mradi huu ni Rainforest Alliance.

Siku ya Kakao na Chokoleti Duniani  huadhimishwa tarehe 1 Oktoba kila mwaka. Siku hii inatokana na wazo kutoka kwa Shirika la Kimataifa la Kakao na Académie Française du Chocolat et de la Confiserie. Ilianzishwa kuhamasisha juu ya hali ya maisha ya wakulima wa kakao kote ulimwenguni katika juhudi za kufanya uchumi wa kakao kuwa endelevu.  Kwa kukuza Sekta ya kiasili ya chokoleti  Itasaidia kuwa na uchumi anuai na pia kusaidia wakulima kupata mapato bora.

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na Ulrich Piest