27 May 2021 Toleo la habari Kutumia mazingira kushughulikia tabianchi

Dunia inahitaji uwekezaji kwa mazingira wa dola trilioni 8.1 kufikia mwaka wa 2050 ili kukabiliana na changamoto za aina tatu duniani

Geneva, Mei 27, 2021 – Jumla ya dola za Marekani trilioni 8.1 zinahitaji kuwekezwa ili kushughulikia mazingira kuanzia sasa hadi mwaka wa 2050 - huku uwekezaji wa kila mwaka ukihitaji kufikia dola za Marekani bilioni 536 kila mwaka kufikia mwaka wa 2050 - ili kufanikiwa kukabiliana na changamoto zinazoingiliana za mabadiliko ya tabianchi, bayoanuai, na uharibifu wa ardhi, kwa mjibu wa ripoti ya Hali ya Ufadhili wa Mazingira iliyotolewa leo.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa uwekezaji wa kila mwaka katika  masuluhisho yanayotokana na mazingira unapaswa kuongezeka mara tatu kufikia mwaka wa 2030 na kuongezeka mara nne zaidi kufikia mwaka wa 2050 ikilinganishwa na uwekezaji wa sasa katika masuluhisho yanayotokana na mazingira wa dola za Marekani bilioni 133 (kwa kuzingatia hali ya mwaka wa 2018).

Waandishi wa ripoti hiyo–iliyochapishwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) na Mradi wa Uchumi wa Uharibifu wa Ardhi (ELD)  ulio chini ya Deutsche Gesellschaft für Internationale Zusammenarbeit (GIZ) kwa ushirikiani na Vivid Economics – inatoa wito kwa Serikali, taasisi za kifedha na mashirika ya biashara kupunguza hili  pengo la uwekezaji kwa kufanya mazingira nguzo wakati wa kufanya maamuzi kuhusu uchumi katika siku zijazo. Wanasisitiza haja ya kuimarisha kwa kasi ufadhili wa masuluhisho yanayotokana na mazingira kwa kufanya mazingira nguzo wakati wa kufanya maamuzi katika sekta ya umma na ya kibinafsi kuhusiana na changamoto katika jamii, ikijumuisha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na changamoto ya bayoanuai.

Kutumia masuluhisho yanayotokana na mazingira kuziba pengo la ufadhili kufikia mwaka wa 2050

Mabadiliko ya kimuundo yanahitajika ili kuziba pengo la kifedha la dola za Marekani trilioni  4.1 kuanzia sasa hadi mwaka wa 2050, kwa kuimarisha uchumi kwa njia endelevu zaidi baada ya janga la Covid-19, na kwa kuondoa ruzuku kwa kilimo hatari na kwa fueli ya visukuku na kuunda sheria zinazotuza wakuzaji wa uchumi. Kuwekeza kwa mazingira kunasaidia afya ya binadamu, wanyama na kuboresha sayari, huboresha maisha, na kubuni nafasi za kazi. Hata hivyo, mazingira kwa sasa hugharamia asilimia 2.5 ya fedha zilizotengewa kuimarisha uchumi baada ya janga la Covid-19. Mitaji ya kibinafsi pia inapaswa kuimarishwa mno ili kupunguza pengo la uwekezaji. Kukuza na kuimarisha mzunguko wa mapato kutoka kwa huduma za mifumo ya ekolojia na kutumia mifumo mbalimbali ya ufadhili kama njia ya kuchanga mtaji wa kibinafsi ni miongoni mwa masuluhisho yanayohitajika kufanikisha jambo hili, ambalo pia linahitaji ushirikiano wa mashirika ya sekta binafsi kukabiliana na hatari kutoka kwa .

 

“Kudidimia kwa bayoanuai tayari kunagharimu uchumi ulimwenguni asilimia 10 ya pato lake la kila mwaka. Ikiwa hatutafadhali masuluhisho yanayotokana na mazingira vya kutosha, tutaathiri uwezo wa nchi kufanya maendeleo kwenye sekta zingine muhimu kama vile elimu, afya na ajira. Ikiwa hatutaokoa mazingira sasa, hatutaweza kufikia maendeleo endelevu, " alisema Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Inger Andersen.

 

“Ripoti hiyo ni wito kwa Serikali, taasisi za kifedha na mashirika ya biashara kuwekeza kwenye mazingira — ikijumuisha upandaji wa miti, kilimo cha kisasa, na uboresaji wa Bahari yetu” alisema, akiongeza kuwa nchi na viongozi wa sekta hii watakuwa na fursa ya kufanya hivyo katika mkutano ujao unaohusu hali ya hewa, bayoanuai, uharibifu wa ardhi na mifumo ya chakula, na katika muktadha wa Muongo wa Umoja wa mataifa wa Kuboresha mifumo ya Ekolojia (2021-2030).

 

Kuwekeza vyema Tafakari, buni, boresha

 Masuluhisho yanayozingatia tu misitu, ikijumuisha usimamizi, uhifadhi na uboreshaji wa misitu, yatahitaji dola za Marekani bilioni 203 kwa jumla ya matumizi ya kila mwaka ulimwenguni, kulingana na ripoti hiyo. Hiyo ni sawa na zaidi ya dola za Marekani 25 kwa mwaka kwa kila raia katika mwaka wa 2021. Ripoti hiyo inatoa wito wa kujumuisha uwekezaji katika hatua za uboreshaji na ufadhili wa hatua za uhifadhi. Hii inaweza kukuza misitu na kilimo cha misitu (mchanganyiko wa uzalishaji wa chakula na upandaji wa miti) kuongezeka kwa eneo la takriban hekta milioni 300 kufikia mwaka wa 2050, ikilinganishwa na mwaka 2020.

Mkutano mkuu ujao kuhusu hali ya hewa, bayoanuai, uharibifu wa ardhi na mifumo ya chakula, na uzinduzi wa Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia tarehe 5 mwezi wa Juni mwaka wa 2021 ni fursa ya kuimarisha kasi ya kisiasa na biashara ili kuimarisha uchumi baada ya janga kwa kuzingatia Mkataba wa Paris na Mfumo wa Bayoanuai Duniani unaotarajiwa baada ya 2020, na kwa hivyo kuwezesha kudhibiti ongezeko la joto lisizidi nyuzijoto 1.5 zaidi kuliko kabla ya viwanda, na vilevile kusitisha na kukabiliana na uharibifu wa bayoanuai.

Kujumuisha mazingira kwenye biashara na uwekezaji

Waandishi wa ripoti hiyo wanasema uwekezaji wa kila mwaka wa sekta binafsi katika masuluhisho yanayotokana na mazingira ulifikia dola za Marekani bilioni 18 katika mwaka wa 2018. Ufadhili wa sekta binafsi unachangia tu asilimia 14, ikijumuisha mtaji unaopatikana kupitia kilimo endelevu usambaji wa misitu, uwekezaji wa sekta binafsi wa hisa zisizo na riba ya kudumu, shughuli za bayoanuai zinazofadhiliwa na sekta binafsi, mtaji kutoka kwa wahisani, ufadhili wa kibinafsi kutoka kwa mashirika ya kimataifa na misitu na masoko mengine ya gesi ya ukaa yanayohusiana na matumizi ya ardhi.

Kwa ufadhili wa tabianchi, uwekezaji wa sekta binafsi unachangia mtaji mwingi (asilimia 56 kulingana na Mpango wa Sera ya Hali ya Hewa). Kuimarisha mtaji kutoka kwa sekta binafsi kwa kufadhili masuluhisho yanayototana na mazingira ni moja wapo ya changamoto kuu ya miaka michache ijayo huku kukiwa na ewekezaji hasa kwenye mazingira ili kuwezesha ukuaji endelevu wa uchumi katika karne ya 21.
 

Wawekezaji, wafanya maendeleo, watengenezaji wa miundombinu ya soko, wateja na walengwa wanaweza kushiriki katika kuunda soko ambapo masuluhisho yanayotokana na mazingira yanakuwa na mbinu mpya za ufadhili, kuimarisha uthabiti wa shughuli za kibiashara, kupunguza gharama au kuchangia sifa nzuri na malengo.

Wakati tayari miradi mingi inayoongozwa na sekta binafsi imeibuka, ripoti hiyo inasisitiza hitaji la kampuni na taasisi za kifedha kuzidi kuwa sehemu ya suluhisho kwa kushirikiana kukabiliana na hatari na kujitolea kuimarisha ufadhili na uwekezaji kwa masuluhisho yanayotokana na mazingira kwa njia kabambe na kwa malengo yaliyo wazi, kwa mda maalum. Ijapokuwa uwekezaji kwenye masuluhisho yanayotokana na mazingira hauwezi kuchukua nafasi ya ukabilianaji mkuu wa gesi ya ukaa katika sekta zote za uchumi, unaweza kuchangia kwa kasi na kwa kiwango kinachohitajika cha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

MAKALA KWA WAHARIRI
 

Kuhusu Mradi wa Uchumi wa Uharibifu wa Ardhi (ELD)
Mradi wa ELD ni mradi wa kimataifa ulioanzishwa katika mwaka wa 2011 na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Jangwa, Wizara ya Ujerumani ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo, na kamisheni ya Ulaya. Inasaidiwa na mtandao mpana wa wabia katika nyanja mbalimbali za maarifa.

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP):

UNEP in mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira ulimwenguni.  Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.

Kuhusu Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF)
Jukwaa la Uchumi Duniani ni Shirika la Kimataifa la Ushirikiano wa Sekta za Umma na Binafsi. Inashirikisha viongozi wa kisiasa, mashirika ya biashara, viongozi wa kitamaduni na viongozi wengine katika jamii ili kuunda ajenda za kimataifa, kikanda na katika sekta.

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Keishamaza Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, UNEP
Waltraud Ederer, Mshauri, Mradi wa ELD
Amanda Russo, Msimamizi wa Makala ya Media, Jukwaa la Uchumi Duniani, +41 79 392 6898