Photo by Jackman Chiu on Unsplash
10 Dec 2020 Toleo la habari Uchunguzi wa mazingira

Watu sita waliosababisha mabadiliko ya kipekee kwa mazingira watuzwa kama Mabingwa wa Dunia

  • Tuzo la Mabingwa wa Dunia linalotolewa na Umoja wa Mataifa ni tuzo la ngazi ya juu linalotolewa kwa heshima ya mazingira. Viongozi wa kipekee kutoka kwa serikali, mashirika ya uraia na sekta binafsi hutuzwa kila mwaka. 
  • Mabingwa wa Dunia hutia moyo, hupigania, huhamasisha na kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto kubwa zinazoikumba dunia kwa sasa.
  • Tuzo la mwaka huu linatolewa kwa washindi katika vitengo vya Mafanikio ya Kudumu,  Motisha na Kuchukua hatua, Uongozi Unaozingatia Sera, Maono ya Ujasiriamali na Sayansi na Ubunifu.

Nairobi, Disemba 11, 2020 - Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) leo lilitangaza washindi sita wa Tuzo la Mabingwa wa Dunia la mwaka wa 2020, tuzo la ngazi ya juu linalotolewa kwa heshima ya mazingira. Washindi walichaguliwa kutokana na mchango wao ulioleta mabadiliko kwa mazingira na kuwa mstari mbele kushawishi watu kuchukua hatua dhabiti kwa niaba ya sayari na wanaoishi ndani yake.

Tangu kuzinduliwa kwake katika mwaka wa 2005,  tuzo la Mabingwa wa Dunia linalotolewa kila mwaka, limetoa umaarufu na kusifia watu walio mstari mbele kupigania mazingira: ikijumuisha wanasayansi chupukizi, viongozi wa kampuni, wakuu wa nchi na mahamasishaji katika jamii.  Tuzo hili husherehekea watu wanaohimiza na wanaoweza kuigwa wanaonyesha kuwa juhudi za mtu mmoja au za kundi la watu zinaweza kuleta mabadiliko duniani.

Akiwapongeza washindi wa mwaka huu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema:Wakati wa ugonjwa mtandavu kote ulimwenguni, chumi ziliporomoka na kuzidisha changamoto kwa mazingira, sasa, kuliko kipindi kingine chochote, tunahitaji kuchukua hatua dhabiti kwa dharura ili kuboresha uhusiano wetu na mazingira. Washindi wa Tuzo la Mabingwa wa Dunia hututia moyo. Wao hutushawishi kutafakari zaidi, kufanyia kazi mawazo yetu kwa kuchukua hatua dhabiti, na kushirikiana kujenga mustakabali mwema."

"Washindi wa mwaka huu wamejizatiti, wamekabiliana na changamoto na kuamua kujitolea kutunza na kuboresha mazingira," alisema Katibu Mkuu Mtendaji wa UNEP Inger Andersen. Mbali na kutia moyo, wao hutukumbusha kuwa suluhu iko mikononi mwetu, na tuna maarifa na teknolojia ya kudhibiti mabadiliko ya tabianchi na kuzuia mifumo ya ekolojia kusambaratika. Ni wakati wa kushughulikia mazingira."

Washindi wa Tuzo la Mabingwa wa Dunia wa mwaka wa 2020 kwa kuzingatia alfabeti ni:

  • Waziri Mkuu Frank Bainimarama kutoka Fiji, aliyetuzwa katika kitengo cha Uongozi Unaozingatia Sera kwa juhudi zake za kimataifa za kushughulikia mazingira na kujitolea kwake kuweka mikakati ya kitaifa ya kushughulikia mazingira
  • Dr. Fabian Leendertz (Ujerumani), alituzwa katika kitengo cha Sayansi na Ubunifu kutokana na uvumbuzi wake kuhusiana na magonjwa kutoka kwa wanyama na kazi yake kwenye One Health
  • Mindy Lubber (Marekani), aliyetuzwa katika kitengo cha Maono ya Ujasiriamali kwa kujitolea kwake kuhimiza wawekezaji kuwekeza kwenye kampuni zisizochafua mazingira na kuwajibisha mashirika ya biashara kushughulikia mazingira na kuwa endelevu
  • Nemonte Nenquimo (Ecuador), aliyetuzwa katika kitengo cha Motisha na Kuchukua Hatua kwa kuwa mstari mbele kushirikiana na jamii za kiasili hali iliyowezesha kusitisha uchimbaji visima kwenye misitu ya Amazon
  • Yacouba Sawadogo (Burkina Faso), aaliyetuzwa pia katika kitengo cha Motisha na Kuchukua Hatua kwa kuwafundisha wakulima njia zake za kiasili zinazojali mazingira za kuboresha mchanga wao na kuwezesha ardhi yao mbovu kutumika kwa kilimo na kupanda misitu barani Afrika

Washindi wa mwaka huu wanashirikisha Profesa Robert D. Bullard (USA) aliyetuzwa katika kitengo cha Mafanikio ya Kudumu kwa kujitolea kwake kuhakikisha kuwa mazingira yanafanyiwa haki.

Kwa kuhamasisha kuhusu kazi muhimu inayofanywa na wanaharakati wa mazingira, tuzo la Mabingwa wa Dunia linalotolewa kutoa motisha kwa watu zaidi na kuchombea watu zaidi kuchukua hatua za kushughulikia mazingira. Kutokana na janga la COVID-19, kutangazwa kwa washindi wa Tuzo la Mabingwa wa Dunia kulifanyika mtandaoni, tunapoelekea Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia, utakaoanza mwanzoni mwa mwaka wa 2021. Kama sehemu ya kampeni ya UNEP’ ya #ForNature (#TutunzeMazingira) kuongezea uzito Kongamano la Umoja wa Mataifa la Bayoanuai (COP 15) litakalofanyika mjini Kunming mwezi wa Mei mwaka wa 2021, na kuimarisha juhudi za kushughulikia tunapoekea kongamano la a Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) mjini Glasgow katika mwezi wa Novemba mwaka wa 2021.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa

UNEP UNEP ni mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira duniani.  Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo. 

Kuhusu Mabingwa wa Dunia

Mabingwa wa Dunia  hutuza viongozi wa kipekee kutoka kwa serikali, mashirika ya uraia na sekta binafsi.Tangu kuzinduliwa kwake katika mwaka wa 2005, Tuzo la Mabingwa wa Dunia  limewatuza washindi 95, ikijumuisha viongozi 24, watu binafsi 57 na mashirika 12. Waliowahi kushinda ni rais mstaafu wa Chile Michelle Bachelet, vuguvugu la vijana wanaokabiliana na mabadiliko ya tabianchi la Fridays for the Future, Mtaalamu wa masuala ya Bahari Sylvia Earle, Mmarekani aliyehudumu kwenye serikali Al Gore, Jumuia ya Kitaifa ya Jiografia, na wengineo.