AFP/ Yasser Al-Zayyat
11 Jul 2023 Tukio Kushughulikia Mazingira

Kadiri hali ya hewa inavyobadilika, dhoruba za mchanga husababisha uharibifu kwa jamii za maeneo ya majangwa

Kukumbwa na dhoruba ya mchanga au vumbi kunaweza kuogofya. Wakati mawimbi ya vumbi yanapozunguka kila kitu kwenye njia yake, tufani hugeuza mchana kuwa usiku na kusababisha uharibifu kwa wanadamu na kwa mazingira.  Mbaya zaidi ni kama tsunami za mchanga.

Dhoruba hizi huathiri takribani watu milioni 330 kote ulimwenguni, kuanzia Jangwa la Sahara hadi Kaskazini mwa China na hadi Australia. 

Idadi hii inatarajiwa kuongezeka.

Mabadiliko ya tabianchi na matumizi mabaya ya ardhi yanapelekea maeneo ukame kupungukiwa na mimea na kupelekea kuenea kwa jangwa na mfululizo wa dhoruba mbaya zaidi za mara kwa mara. 

Umoja wa Mataifa mapema mwakani ulitennga Julai 12 kuwa maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Kimataifa ya Kukabiliana na Dhoruba za Mchanga na Vumbi. Hatua hiyo ililenga ili kuhamasisha kuhusu vitisho vinatokana na vipupwe hivi na kuchochea juhudi za kimataifa za kukabiliana na hali hii.

"Sio lazima tujiuzulu kwa mustakabali ambapo jamii katika mazingira kame zitakumbwa daima na dhoruba za vumbi," alisema Doreen Robinson, Mkuu wa Tawi la Bayoanuai na Ardhi la Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP). "Kwa kuboresha mandhari yaliyokauka na kupunguza kiwango kikubwa cha uzalishaji wa gesi ya ukaa, tunaweza kupunguza utokeaji wa dhoruba kubwa na kuimarisha maisha ya mamilioni ya watu."

Kwa kuzingatia haya, hapa kuna kila kitu unachohitaji kujua kuhusu dhoruba za mchanga na vumbi, na jinsi binadamu wanavyoweza kudhibiti athari zake haribifu.

Ni nini chanzo cha dhoruba za mchanga na vumbi?

Tufani hizi hutokea wakati ambapo upepo mkali unapokutana na udongo kavu au uliokauka, na kuinua kiasi kikubwa cha mchanga na vumbi angani. Baada ya kupeperushwa hewani, mchanga na vumbi havikai mahali pamoja bali husafirishwa mamia au hata maelfu ya kilomita.

Vyanzo vikuu vya vumbi hii ya madini ni maeneo kame ya Kaskazini mwa Afrika, Rasi ya Arabia, Asia ya Kati na Uchina.   Australia, Marekani na Afrika Kusini huchangia kidogo, lakini bado ni wachangiaji muhimu.

Dhoruba za mchanga na vumbi zinazidi kutokea mara nyingi?

Ndiyo. Shughuli za binadamu, kama vile ukataji miti, kulisha mifugo kupindukia na matumizi ya maji kupita kiasi, vinasababisha jangwa kuenea na kuongeza uwezekano wa dhoruba za mchanga na vumbi kutokea. Mabadiliko ya tabianchi - ambayo yanapelekea ukame na joto kali zaidi - huzidisha matukio haya. 

Katika baadhi ya maeneo, vumbi jangwani imeongezeka maradufu katika karne ya 20, na hivyo kuongeza uwezekano wa dhoruba za mchanga na vumbi kutokea. 

Athari za dhoruba za mchanga na vumbi ni zipi?

Zinaweza kuwa na athari mbaya zaidi kwa kilimo na viwanda.  Kaskazini mwa Uchina pekee zilisababisha hasara za kiuchumi za takribani dola bilioni 1 katika miaka mitatu tu.

Zaidi ya kuathiri biashara vibaya, dhoruba za mchanga na vumbi pia zinaweza kusababisha magonjwa anuai yanayoathiri mfumo wa kupumua wa binadamu.

Takribani asilimia 40 ya erosoli - mkusanyiko wa chembechembe ndogo - zinazopatikana katika sehemu ya chini zaidi ya anga Duniani ni chembechembe za vumbi zinazobebwa na upepo. Chembe hizo zikinaswa kwenye pua, mdomo na sehemu ya juu ya mfumo wa kupumulia, zinaweza kusababisha matatizo kama vile pumu au nimonia.

Chembechembe ndogo zaidi zinaweza kupenya hata zaidi, na kufikia mkondo wa damu na kuathiri viungo vyote.  Tathmini ya 2014 inakadiria kuwa vifo vya mapema 400,000 vilisababishwa kutokana na kukumbana na chembechembe za vumbi.

Chembechembe za vumbi pia zinaweza kutumika keeneza magonjwa ya kuambukizana. Meningococcal meningitis ni maambukizi ya bakteria kwenye ubongo.  Ikiachwa bila kutibiwa husababisha vifo kwa asilimia 50 ya visa. Hali hii hutokea zaidi katika "ukanda wa meningitis" Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika, ambapo watafiti wamehusisha ugonjwa huo na vumbi.

Kando na athari kwa afya ya binadamu, dhoruba za mchanga na vumbi zinaweza kuharibu mimea, kuua mifugo, kuharibu mashine na kuathiri safari za ndege.

Watu wanaweza kufanya nini ili kuzuia dhoruba za mchanga na vumbi, au kupunguza athari zake?

Tukio hili ni gumu kudhibiti moja kwa moja: ukame au ukataji miti katika sehemu moja ya dunia unaweza kupelekea dhoruba za mchanga katika sehemu nyingine. Lakini watu wanaweza kudhibiti mambo yanayosababisha ardhi kukauka na vumbi kukusanyika angani.

Katika maeneo ambapo dhoruba za mchanga na vumbi huanzia, mataifa yanaweza kuboresha ardhi kwa kutumia maji haba vizuri, kutunza udongo dhaifu wa juu na kupanda mimea zaidi, ikiwa ni pamoja na kupanda vichaka na miti ya kiasili.  Haya yote husaidia kuhifadhi maji katika ardhi na, kwa hivyo, mchanga na vumbi kidogo huundwa.

Katika maeneo kame, mataifa yanaweza pia kusaidia wakulima kuzalisha chakula bila kutumia njia ya kuondoa mimea ardhini na kulisha mifugo kupindukia, na kutoa fursa kwa udongo kupumzika na kuimarika.

Kwa kuzingatia uhusiano kati ya mabadiliko ya tabianchi na kuenea kwa jangwa kwa kutambaa, ulimwengu sharti pia ujitahidi kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa unaochangia kwa janga la mazingira.  Tayari dunia inashuhudia joto la nyuzijoto 1.1 zaidi kuliko ilivyokuwa nyakati za kabla ya viwanda na kadiri joto linavyoendelea kupanda, kutakuwa na ukame zaidi hali itakayochangia zaidi dhoruba za mchanga na vumbi.

Hatimaye, mataifa yanapopambana na vyanzo vya dhoruba hizi, yanaweza kuendelea kuwekeza katika mifumo ya maonyo ya mapema ambayo huwatahadharisha watu walio hatarini kuhusu dhoruba zinazokuja.  Mambo haya yanaweza kuokoa maisha na kupunguza athari mbaya kwa uchumi.

Kuhusu Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia wa 2021–2030
Baraza la Umoja wa Mataifa lilitangaza Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia wa 2021–2030, unaoongozwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa pamoja na wabia wake unashughulikia mifumo ya ekolojia ya maeneo ya nchi kavu,pwani na bahari. Mwito kwa jamii ya kimatifa kuchukua hatua, Muongo wa UN huungwa mkono na wanasiasa, utafiti wa kisayansi, na ufadhili ili kuimarisha uboreshaji. Jifahamishe zaidi hapa.